Na: Hendrick Msangi
JUMLA ya Wasichana 96,481 wenye umri wa Miaka 9 hadi 14 wanatarajiwa kupata chanjo ya Human Papillomavirus (HPV) ili kuwakinga kupata saratani ya Mlango wa Kizazi.
Hayo yameelezwa wakati wa uzinduzi wa chanjo ya HPV na shughuli jumuishi za lishe Halmashauri ya Wilaya ya Geita uliofanyika katika shule ya msingi Ihumilo kata ya Nkome Aprili 24, 2024 huku Kauli Mbiu ya wiki ya chanjo kwa mwaka 2024 ikisema, Jamii iliyochanjwa, Jamii yenye Afya.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi ambaye ni Mhe Masumbuko Nsembe Diwani wa Kata ya Nkome, Dkt Maro Willium kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Geita amesema zoezi la utoaji wa chanjo limeanza kutekelezwa Aprili 22, 2024 ambapo linatarajiwa kumalizika ifikapo Aprili 28, 2024 likienda sambamba na huduma za afua za lishe, huku lengo likiwa ni kuwafikia wasichana 96,481.
Akiendelea kuzungumza katika Uzinduzi wa Chanjo ya HPV na shughuli jumuishi za Lishe , Dkt Maro amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo itaendelea kuelimisha jamii ili kutambua umuhimu wa kuwapeleka watoto kliniki kwa lengo la kupata chanjo na elimu. “Serikali itaendelea kutoa elimu ya lishe kupitia klabu za afya na lishe mashuleni na kuendelea kufuata sheria mbalimbali zilizotungwa ili kuhakikisha haki za watoto zinalindwa” Amesema Dkt Maro.
Mhe Masumbuko Nsembe Diwani wa Kata ya Nkome,amewataka wanafunzi wa shule ya msingi Ihumilo kuwa mabalozi kwa wenzao ambao hawajapewa chanjo huku akiwapongeza walimu kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa wataalam wa afya katika kuwaelemisha wanafunzi mabinti juu ya umuhimu wa chanjo ya HPV
Mhe Nsembe akipokea maelezo kutoka kwa Wataalam wa Afya baada ya uzinduzi wa wiki ya chanjo HPV katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kata ya Nkome
Akizungumza katika Uzinduzi huo, mgeni rasmi Mhe Masumbuko Nsembe Diwani wa Kata ya Nkome amewataka wasichana wa shule ya msingi Ihumilo ambapo Uzinduzi huo umefanyika kuendelea kuwa mabalozi wazuri kwa wasichana wenzao wenye umri wa miaka 9 hadi 14 ambao hawajapata chanjo hiyo kuona umuhimu wa kupata chanjo ya HPV kwa lengo la kuwalinda na Saratani ya Mlango wa Kizazi.
Aidha Mhe Nsembe amewapongeza walimu kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa wataalam wa afya katika kuwaelemisha wanafunzi mabinti juu ya umuhimu wa chanjo hiyo ambayo serikali inahakikisha inawafikia mabinti wote wanaotakiwa kuchanjwa.
Naye Mratibu wa Chanjo Wilaya ya Geita ndugu Jalion Manyi amesema zoezi la Chanjo linaendelea katika kata zote 37 za Halmashauri ya wilaya ya Geita huku jumla ya vituo 60 vya kutolea huduma vikiendelea na zoezi la utoaji wa Chanjo ya HPV. “Tunategemea kufikia jumla ya shule za msingi 234 na sekondari 74 tukishirikiana na walimu pamoja na wataalam wa afya kwenye vituo vyote vya afya na kwa wale wasichana ambao wapo mtaani watapata huduma kupitia vituo maalum vilivyotengwa katika kila kata.” Amesema Jalion Manyi.
Mratibu wa Chanjo Wilaya ya Geita , Jalion Manyi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na walimu pamoja na wataalam wa afya kwenye vituo vyote vya afya ili kufikia lengo la kuwachaja wanafunzi mabinti katika shule za msingi 234 na sekondari 74 na wale ambao wapo mtaani kwani jumla ya vituo 60 vinatoa huduma ya chanjo ya HPV ili kuwakinga mabinti wenye umri wa miaka 9 hadi 14 dhidi ya maambukizi ya saratani ya Mlango wa Kizazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Wakati huo huo Mwanafunzi wa darasa la sita, Elizabeth John mwenye umri wa miaka 13 ameshukuru kwa kupata chanjo hiyo na kusema atawahamasisha na wasichana wengine ili kupata chanjo hiyo muhimu ya kinga dhidi ya maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi.
Serikali Kupitia Wizara ya Afya imepanga hadi kufikia mwezi Disemba 2024 iwe imefikia jumla ya wasichana Milioni 4,841,298 wenye Umri wa Miaka 9 hadi 14 kwa kuwapa dozi moja ya chanjo ya Human Papillomavirus (HPV) baada ya kujiridhirisha kuwa chanjo hiyo haina madhara na kwamba dozi moja inatosha kutoa kinga kamili dhidi ya maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea kuishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwezesha vifaa vya kupima na kutibu mabadiliko ya awali ya Saratani ya Mlango wa Kizazi mpaka ngazi ya Zahanati ili kuwa na watanzania wenye afya bora kwa maendeleo ya Taifa lao.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa