Wanafunzi wametakiwa kutumia Tehama kwa lengo la kuongeza maarifa ya kitaaluma kuliko kutumia kwa mambo yasiyo ya msingi kwa kuwa Tehama ikitumika vibaya inaweza kuwa chanzo cha matatizo mbalimbali ikiwemo mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Hayo yamebainishwa na Timu ya Uhamasishaji na matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA) Wilaya ya Geita wakati ikitoa mafunzo ya matumizi sahihi yaTEHAMA hii leo Septemba 28 kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Geita (GESECO)shuleni hapo.
Akiwawezesha wanafunzi hao Bw.Msajigwa Alfred Mkurugenzi wa Taasisi ya Infodigtech For Empowerment amesema kuwa Matumizi ya TEHAMA ni muhimu sana kwa wanafunzi na inaweza kuwasaidia katika tafiti,elimu kwa njia ya mtandao,kutafuta machapisho ya kujifunzia na hata majadiliano ya mtandaoni.
Ameendelea kusema kuwa endapo TEHAMA itatumiwa tofauti na wanafunzi hao kwa matumizi yasiyo ya msingi kama kuangalia picha zisizofaa, inaweza kuchangia kuporomosha maadili yetu suala lisilo na faida katika maisha ya mwanafunzi.
Aidha Mwezeshaji Frank Makonda ambaye pia ni Afisa TEHAMA wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita amesema kuwa ukuaji wa Sekta hiyo ya TEHAMA ni faida kwa wanafunzi hao katika kujisomea kwa kuwa kwa sasa kuna Maktaba mtandaoni inayowawezesha kupata maarifa mbalimbali yanayowahusu.
Amesema kuwa Maktaba mtandaoni inapunguza changamoto za uhaba wa Maktaba kwa kuwa si lazima ufike maktaba kujisomea, kwa kuwa unaweza kupata machapisho mbalimbali kwa njia ya mtandao huku akiwahamasisha wanafunzi hao kutumia fursa hiyo kujifunza kwa urahisi.
Kwa upande wake mwezeshaji Michael Mpamwa kutoka Infodigtech For empowerment amewataka wanafunzi hao kujizuia wenyewe kutumia vibaya TEHAMA kabla ya kuzuiwa na sheria huku akiwatahadharisha kuwa sheria kali zinaendelea kuchukuliwa kwa wanaoitumia vibaya mitandao.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Zachari Ezekiel Jembe Mwanafunzi wa kidato cha tano HKL amesema kuwa elimu hiyo imemsaidia kuyafahamu madhara mbalimbali ya kutumia vibaya mitandao lakini kufahamu adhabu anazoweza kuzipata mtu anayetumia vibaya TEHAMA.
Semina hiyo ni mwendelezo wa kuwafikia wadau mbalimbali na kuwaelimisha matumizi sahihi ya TEHAMA katika kuadhimisha wiki ya TEHAMA Wilayani Geita, ikiwa ni Utekelezaji wa kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu inayosema ‘’TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu itumie kwa usahihi na uwajibikaji’’suala linalowataka wadau wote wa TEHAMA zikiwemo taasisi zilizopewa dhamana hiyo kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi kwa maendeleo ya nchi yetu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa