Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeongoza kati ya Halmashauri Sita za Mkoa wa Geita katika Matokeo ya Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika Oktoba 5, 2024.
Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 zilianza Mkoani Kilimanjaro Aprili 2, 2024 ambapo Mhe Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) alizindua mbio hizo na kuhitimishwa Oktoba 14, 2024 jijini Mwanza na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), alipozindua mbio za Mwenge wa Uhuru Aprili 2,2024 katika uwanja wa chuo kikuu cha Ushirikia Moshi. (picha kutoka maktaba)
Akizungumza na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Alex Herman ameelezea furaha aliyo nayo kwa matokeo hayo na kusema kazi haikuwa ndogo.
Mratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Alex Herman akiwa kwenye mbio za Mwenge wa Uhuru uliokimbizwa Wilayani Geita Oktoba 5, 2024 na kupelekea Halmashauri ya Wilaya ya Geita kushika nafasi ya 17 Kitaifa.
“Sikutegemea kwa kweli kutokana na misukosuko na changamoto nyingi sana wakati wa maandalizi hayo ila Mwenyezi Mungu amewezesha na hatimaye tumekuwa washindi,” amesema Alex.
Aidha Mratibu huyo ametoa shukrani kwa kamati zote zilizowezesha mapokezi ya mbio za mwenge wa uhuru 2024.”Kipekee sana nipende kuishukuru kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Mh. Hashim Komba, Mkurugenzi Mtendaji Ndg.Karia Rajabu Magaro,viongozi wa chama na dini, wakuu wa idara na vitengo, Taasisi mbalimbali ikiwepo Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Geita (GEUWASA), wadau mbalimbali kwa namna walivyotoa michango yao pamoja na wananchi wote kwa jitihada na kuonesha ushirikiano kipindi chote cha maandalizi hadi tulipokabidhi Mwenge wa Uhuru Halmashauri ya Buchosa Wilayani Sengerema Oktoba 6,2024.” ameongeza Alex.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya Geita Ndg Karia Rajab Magaro (kulia) akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji Geita Mji Ndg Yefred Miyenzi Oktoba 5, 2024 katika viwanja vya shule msingi Bugulula
Pamoja na kuwa ya kwanza Kimkoa, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeshika nafasi ya 6 kwa kanda yenye halmashauri 45 na kushika nafasi ya 17 kitaifa kati ya Halmashauri 195 zilizokimbiza Mwenge wa Uhuru 2024.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Martine Shigela(Kulia) akimkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Said Mtanda Oktoba 6,2024 Halmashauri ya Buchosa Wilayani Sengerema baada ya kumaliza kukimbizwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Mwenge wa Uhuru ni chombo kilichoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961 ikiwa ni tunu na ishara ya kuwepo kwa Taifa huru la Tanganyika.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zilianza rasmi mwaka 1964 baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwenge wa uhuru umekuwa kichocheo kikubwa katika kuimarisha uhuru wa Taifa la Tanzania,umoja wa kitaifa, kudumisha amani, kulinda Muungano na kuhamasisha maendeleo ndani na nje ya taifa la Tanzania.
Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2024 imesema “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan akipokea Mwenge wa Uhuru Oktoba 14, 2024 kutoka kwa Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndg Godfrey Eliakimu Mzava Kwenye hafla ya kilele Cha mbio hizo Uwanja wa CCM Kirumba Mkoani Mwanza . (picha kutoka Maktaba)
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa