Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), leo Mei 12 imetangaza mabadiliko kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika badae mwezi Oktoba mwaka huu kwa kuongeza majimbo mawili mapya Mkoani Geita.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari Mkoani Dodoma, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Jacobs Mwambegele amesema kuwa, kwa upande wa Mkoa wa Geita, majimbo yaliyoongezwa ni pamoja na Jimbo jipya la Uchaguzi la Katoro, lililotokana na Jimbo la Uchaguzi, Busanda, pamoja na Jimbo jipya la Chato Kusini, lililotokana na Jimbo la Chato.
Mapema mwezi Februari 28 mwaka huu, tume hiyo ilipokea rasmi maombi ya kugawanywa kwa Jimbo la Busanda kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, na mnamo tarehe 23 Aprili, tume hiyo ilifanya kikao na wadau wa uchaguzi kutoka Halmshauri ya Wilaya ya Geita , kwa lengo la kujiridhisha kuhusu mchakato wa kugawa jimbo hilo kama ulifuata taratibu na vikao vya kisheria.
Pamoja na vigezo vya ugawaji wa majimbo vilivyoainishwa, Tume imezingatia zaidi baadhi ya vigezo ilivyovipa kipaumbele, likiwemo suala la idadi ya watu, ambapo kwa majimbo ya mjini, kigezo kilikua ni kuanzia watu 600,000, na kwa majimbo ya vijijini ilikua ni kuanzia watu 400,000.
Jaji Mwambegele amesema pia ni muhimu kwa wananchi kuzingatia mabadiliko hayo ya maeneo ya uchaguzi ili waweze kutumia haki yao ya msingi ya kushiriki kugombea na kupiga kura siku ya kupiga kura.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa