Na. Michael Kashinde
Wananchi wameshauriwa kutoa taarifa kuanzia ngazi za msingi wanapokutana na changamoto mbalimbali ikiwemo za migogoro katika familia na masuala ya ukatili, kwa kuwa Serikali imeweka miundombinu rafiki inayoweza kuwaongoza kujua wapi wanaweza kupata huduma ya msaada kulingana na uhitaji wanaokuwa nao.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi. Enedy Mwanakatwe akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Nyarugusu Desemba 14, 2022 wakati wa kuhitimisha kambi ya siku moja ya msaada wa kisheria katika kata ya Nyarugusu.
Bi. Mwanakatwe amesema kuwa kuna haja ya kuendelea kutoa Elimu kwa jamii na kuwaunganisha na sehemu sahihi ambapo wanaweza kupata huduma kulingana na mahitaji yao huku akiwahamasisha wananchi hao kutumia ngazi za chini kupata suluhu ya migogoro ya kifamilia ikiwemo mabaraza ya wazee katika ngazi za Kata.
Kwa upande wake Majaliwa Yohana kutoka kitengo cha Sheria Halmashauri ya Wilaya ya Geita akizungumza na wananchi hao amesisitiza kutumia mabaraza ya usuluhishi kutatua migogoro hiyo badala ya kukimbilia kuripoti vituo vya Polisi ambapo wakati mwingine panakuwa sio sehemu sahihi ya wao kupata suluhu ya migogoro yao ya kifamilia kama ambavyo wangeweza kupata suluhu katika mabaraza hayo.
Jackson Chami Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Geita ametumia nafasi hiyo kuongea na wananchi hao huku akiwakumbusha kutofumbia macho vitendo vya ukatili hasa kwa watoto, ambapo pia amesisitiza kuwa manyanyaso na ukatili havivumiliki hivyo ni wajibu wa jamii kukemea na kutoa taarifa haraka pale wanapoona watu wananyanyasika au kufanyiwa vitendo vya ukatili katika maeneo yao.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyarugusu Mhe. Swalehe Juma Msene akizungumza na wananchi hao amewataka kuendelea kujitokeza kwa wingi yanapotokea masuala kama hayo ya elimu ya msaada wa kisheria ili kuendelea kuwaongezea wananchi hao uelewa wa masuala ya haki mbalimbali za msingi, ambapo pia ameishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuwatumia wataalamu hao kuwafikia wananchi kwenye maeneo yao na kuwapatia huduma hiyo.
Wananchi mbalimbali katika Kata ya Nyarugusu wamejitokeza kupata elimu na msaada wa kisheria kutoka kwa wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita walioweka kambi ya siku moja katika kata hiyo kwa ajili ya shughuli hiyo.
Aidha wamepatiwa ushauri na maelekezo kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo migogoro ya ndoa na kutelekeza watoto, migogoro ya ardhi, masuala ya mirathi, masuala ya talaka na haki mbalimbali za binadamu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa