Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Martine Shigela ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kupata hati safi.
Mhe. Martine Shigela akizungumza katika mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Leo Juni 26, 2024
Mhe Shigela ametoa pongezi hiyo leo Juni 26, 2024 katika mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani wa kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Mkutano huo uliofanyika makao makuu ya Halmashauri Nzera, Mhe. Shigela alisema mwakajana Halmashauri haikupata hati safi,na kwamba kulikuwa na makando kando mengi yaliyosababishwa na miradi iliyotekelezwa na CSR.
Amesema kwasasa wanafanya maboresho kwenye CSR ikiwemo uwezekano wa Halmashauri kufanya taratibu za manunuzi zenyewe na mgodi uweze kulipa, ndiyo maana mwaka huu wa fedha hawajasaini mpango wa CSR kwasababu waliandika barua kwa Waziri Mkuu, Waziri mwenye dhamana ya Madini, Waziri wa TAMISEMI pamoja na Waziri wa fedha kuomba mabadiliko ya kanuni ya CSR ili kuziruhusu Halmashauri zifanye utaratibu wa kuwapata wakandarasi wa kutekeleza hiyo miradi.
amesema utaratibu wa Sasa unaotekelezwa na mgodi, unakwenda taratibu sana, na kwamba mgodi hauwezi kuacha shughuli zake za kufanya manunuzi yake, na kufanya manunuzi ya miradi ya Serikali.
" kwahiyo kwa vyovyote vile, Mgodi unaweka vipaumbele vya kufanya manunuzi ya kuisaidia Mgodi" alisema RC Shigela.
amesema suala hilo likimalizika, Serikali itakuwa imeondokana na kero ya miradi kuchelewa.
Vile vile Mkuu wa Mkoa, Shigela ameipongeza Halmashauri kwa kuwa na jengo zuri la utawala pamoja na ukumbi mzuri wa mikutano ambapo pia alimshukuru Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kuhakikisha majengo ya utawala ya Halmashauri yanakamilika.
Akizungumzia ripoti ya CAG amesema Halmashauri imeonesha madhaifu kwenye maeneo ya fedha hususani kwenye mapato na matumizi ambapo nyaraka nyingi hazijaonekana pamoja na mapato ambayo hayajawekwa kwenye akaunti hivyo amewasihi watendaji wa Serikali jambo hilo kutojirudia tena.
Amesema ameshamuelekeza Katibu Tawala Mkoa, kila baada ya miezi mitatu watakuwa wanafanya vikao vya kujadili mapato na matumizi na watakuwa wanaenda kipengele kwa kipengele na kwamba taarifa za Mkaguzi wa ndani ziwe zinawasilishwa ili wabaini ni nani anayechangia Halmashauri kuwa na hoja nyingi ili hatua zichukuliwe
Pia ameitaka kamati ya fedha kuhakikisha mambo hayo hayajitokezi katika siku zijazo.
Baadhi ya Madiwani wakiwa katika mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Leo Juni 26, 2024.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Geita, Shigela amesema mwaka huu 2024 kuna uchaguzi, pamoja na mwaka kesho 2025, hivyo ni vizuri kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha, kuhakiki taarifa zao na kuwanadi Wagombea wazuri ili uchaguzi uende vizuri.
Mkaguzi Mkuu wa Nje wa Hesabu za Serikali Mkoa Geita CPA Richson Ringo amesema endapo menejimenti ya Halmashauri itafuatilia na kuzingatia hayo yaliyoshauriwa, ni imani yao kama wakaguzi kuwa hoja hizo zitafungwa kwa muda mfupi ujao na taarifa itawarudia kujua hali halisi ambacho kimefanyika.
Amesema katika uhakiki wa majibu hayo waliyofanya zipo kasoro mbalimbali zinazosababisha hoja kuendelea kubakia katika vitabu vya Halmashauri kwahiyo wanasisitiza menejimenti ifanye kila linalowezekana kutafuta majibu na nyaraka ambazo zimehojiwa ili hoja hizo waweze kuzifunga.
"Na hili linaweza kufanyika kwa siku za karibuni kwasababu tayari tumeshaanza pangokazi wa ukaguzi wa 2023/2024 kwahiyo majibu hayo kama yatakuwa yameandaliwa vizuri wakaguzi watakapofika kwa ajili ya ukaguzi itakuwa ni fursa nzuri ya menejimenti kupata huduma ya uhakiki wa majibu hayo" alisema CPA Ringo.
Jambo lingine alilosisitiza ni kwamba ili kuepukana na mlundikano wa hoja, menejimenti kutoa ushirikiano wa kutosha vipindi vyote vya ukaguzi na pale ambapo hoja zinaibukiwa katika hatua ya awali ziweze kupatiwa majibu sahihi ili ziweze kufungwa kabla ya kuendelea na hatua zingine za ukaguzi na hatimae kusababisha kuangukia kwenye mrundikano wa hoja.
"endapo kama Kila kiongozi na Mkuu wa Idara, atatimiza wajibu wake wakati wa ukaguzi tunaimani kwamba tutakuwa na hoja chache ambazo pengine ni zile za kisera ambazo siyo rahisi menejimenti kuzijibu kwa wakati wa ukaguzi, lakini kama ushirikiano utakuwa hafifu basi nadhani kwamba tutaendelea na aina hii ya hoja nyingi ambazo zinakuwa katika vitabu vyetu na mwisho wa siku zinakuwa ngumu kujibika" alisema CPA Richson.
Naye Katibu Tawala Mkoa Geita, Mohamed Gombati ameipongeza Halmashauri kwa kupata hati safi.
Katibu tawala Mkoa wa Geita Mohamed Gombati akizungumza katika mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Leo Juni 26, 2024
pamoja na pongezi amewaomba watumishi kuendelea kuimarisha ushirikiano huo na kuongeza kwamba mwenendo wa hoja umezidi kuongezeka na kazi ya kujibu hoja bado ni ndogo.
amesema mwaka Jana kulikuwa na hoja tisa (9) wakajibu tatu (3) na mwaka huu 18 wamejibu 3 hivyo ametoa msisitizo kwa wataalamu kuzingatia sheria ili wasizalishe hoja.
Amesema mwaka huu wa fedha unaoenda kuanza wajitahidi kujibu hoja zote ziishe na wabakize hoja za kisera.
Amesema wapunguze hoja na kwamba wabaki kwenye tarakimu moja na zisizisi hoja kumi.
Pia Katibu tawala Gombati, ameipongeza Halmashauri katika ukusanyaji wa mapato ambayo mpaka Sasa umefikia asilimia 105%.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa