Na. Michael Kashinde
Katika kukabiliana na changamoto ya idadi kubwa ya watu wanaokuja kujifungua katika kituo cha Afya Katoro, inayopelekea kuwa na uhaba wa vitanda vya kulalia wagonjwa hao, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imekabidhi vitanda 20 kati ya 50 vinavyotengenezwa kwa ajili ya Kituo hicho cha Afya.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vitanda hivyo, magodoro, na mashuka yake Novemba 3, 2022 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Adv. John Paul Wanga amesema kuwa baada ya Halmashauri kubaini changamoto hiyo ikaanza mapema mchakato wa kupata vitanda 50 ambapo vitanda 20 tayari vimekabidhiwa katika kituo hicho cha Afya huku vingine 30 vikiendelea kukamilishwa.
Adv. Wanga ameendelea kusema kuwa mchakato wa kupeleka vitanda katika kituo cha Afya Katoro haujafanyika baada ya vyombo vya habari kuripoti uhaba wa vitanda katika kituo hicho, bali ni mchakato ambao ulianza mapema ambapo hata wakati vyombo hivyo vikitoa taarifa hizo tayari taratibu za utengenezaji wa vitanda hivyo zilikuwa zikiendelea.
Ameendelea kusema kuwa kama ambavyo baadhi ya wagonjwa walioongea na vyombo hivyo vya habari walivyoiomba Serikali kuwaletea vitanda katika wodi ya wazazi katika kituo hicho, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwahudumia wananchi kwa kuwatatulia kero mbalimbali kama hizo huku akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan ambaye katika utawala wake ameendelea kuboresha huduma mbalimbali kwa wananchi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya Geita Dr. Modest Buchard amesema kuwa kituo hicho cha Afya kimekuwa kikiwahudumia watu wengi ambao wengine wanatoka maeneo ya nje ya kata ya Katoro ikiwemo eneo la Buseresere ambalo ni eneo la Wilaya ya Chato, hali inayochangia kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa kuzidi uwezo wa hadhi ya Kituo cha Afya.
Dr. Buchard amefafanua kuwa huduma bora zinazotolewa katika kituo hicho cha Afya zimekuwa zimekuwa zikiwavutia watu kuja hapo wakitoka katika maeneo mbalimbali ambapo kwa siku kituo hicho kinahudumia idadi ya wazazi 30 mpaka 40 huku akiishukuru Serikali kwa kuliona hilo na kutoa fedha kwa ajili ya kujenga Hospitali kubwa Katoro yenye hadi ya Wilaya.
Akizungumzia kukabidhiwa kwa vitanda hivyo Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Katoro Zakayo Sungura ameshukuru kupokea vitanda hivyo ambavyo amesema vitakwenda kupunguza kama sio kumaliza kabisa changamoto hiyo huku akitoa takwimu kuwa Kituo hicho cha Afya kwa kipindi hiki cha miezi mitatu mfululizo kimekuwa kikihudumia idadi ya wazazi 900 hadi 1000 kwa mwezi.
Mwongozo wa kituo cha Afya unaonyesha kila kituo kinapaswa kuwa na vitanda visivyozidi 50 ambapo kabla ya kukabidhiwa vitanda 20 katika Kituo hicho cha Afya tayari kulikuwa na jumla ya vitanda 66 na baada ya makabidhiano hayo kituo hicho kimekuwa na jumla ya vitanda 86 hali inayoonyesha kuwa Halmashauri imeendelea kupambana kuhakikisha inawahudumia wahitaji hao licha ya changamoto inazokabiliana nazo suala ambalo linadhihirisha kuwa ni kweli uhitaji wa Hospitali ya Wilaya katika Kata ya Katoro ni la muhimu.
Aidha katika kupata utatuzi wa kudumu katika kukabiliana na changamoto hiyo Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea na ujenzi wa hospitali yenye hadhi ya Wilaya katika kata ya Katoro ambayo inatazamwa kuwa msaada mkubwa katika kukabiliana na changamoto hiyo ya idadi kubwa ya wagojwa katika Kitua cha Afya Katoro.
Vitanda hivyo vimekabidhiwa katika kituo hicho cha Afya Katoro siku mbili tu baada ya Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Cha Mapinduzi Wilaya ya Geita kujitolea kufanya usafi katika kituo hicho na kubaini changamoto hiyo ambapo kwa wakati huo Halmashauri ya Wilaya ya Geita ilikuwa ikiendelea na taratibu za kuleta vitanda hivyo ambavyo vimekabidhiwa siku mbili baadae.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa