Waheshimiwa Madiwani pamoja na watendaji wa kata zote za Halmashauri ya Wilaya ya Geita, wamepatiwa mafunzo maalumu leo tarehe 23 februari, 2022 ya kuwaongezea uelewa kuhusu utekelezaji wa zoezi la anwani za makazi na postikodi.
Mafunzo hayo yametolewa na kamati ya zoezi la anwani za makazi na postikodi kwenye baraza la madiwani maalumu lililofanyika makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita Nzera.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Hongera Edward amesema Serikali kupitia sera ya Taifa ya posta ya mwaka 2003, imedhamiria kuanzisha mfumo wa anwani zinazoendana na majina ya mitaa ambapo watu binafsi na maeneo ya biashara yatatambulishwa kwa kutumia majina ya maeneo yaliyopo pamoja na postikodi yao, ikiwa ni utekelezaji wa dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2025, yenye lengo la kuwaondoa watanzania kwenye umaskini na kuinua ubora wa maisha yao.
Zoezi la anwani za makazi na postikodi linatekelezwa kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ikishirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambapo linatakiwa kukamilika kabla ya mwezi mei 2022, huku halmashauri ya wilaya ya Geita ikipanga kukamilisha zoezi hilo aprili 8 mwaka 2022.
Aidha kukamilika kwa zoezi hilo kutawezesha kufanyika kwa sensa ya watu na makazi zoezi linalotarajiwa kufanyika kuanzia mwezi Agosti, 2022.
Miongoni mwa mambo waliyofundishwa madiwani pamoja na watendaji hao wa kata ni pamoja na maana ya mfumo wa anwani za makazi na postikodi, manufaa ya mfumo wa anwani za makazi, vigezo vya uundaji wa majina ya barabara na mitaa, utaratibu wa utoaji wa jina la barabara au mtaa.
Mambo mengine ni taratibu za kufuatwa, vibao vya majina ya barabara au mtaa, utoaji na ubadilishaji wa majina ya barabara au mtaa, majina yasiyopendeza kimaadili, majina yenye viashiria vya kuharibu amani, utulivu na umoja wa kitaifa pamoja na uwekaji wa miundombinu ya anwani za makazi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Charles Kazungu amewataka wajumbe wa kamati ya zoezi la anwani za makazi na postikodi kuzingatia mawazo yaliyotolewa na madiwani hao ili kazi iwe rahisi na nzuri zaidi.
Mheshimiwa Kazungu amesema wao kama madiwani wanalo jukumu kubwa la kwenda kuhamasisha wananchi ili zoezi litakapoanza wawe na uelewa mzuri.
Ameomba kila diwani katika kata yake na wale wa viti maalumu kutambua kwamba wanalo jukumu la kwenda kuhamasisha wananchi kuelewa zoezi hilo na kuwataka watendaji wa kata kusimamia kwa weledi zoezi hilo.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Geita Wilson Shimo amewataka watendaji wote kuendelea na zoezi hilo kwa kasi bila kubagua kundi lolote ikiwemo watu wenye ulemavu na Taasisi yoyote kuanzia ngazi za mwanzo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa