Na. Michael Kashinde
Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa shule mpya za sekondari 23 kutoka kiasi cha bilioni 5 na milioni 340 (Tshs. 5,340,000,000/=) zilizotolewa na Serikali kuu kupitia TAMISEMI kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 267 vya madarasa katika shule 39 kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupitia vikao vyake Maalumu vya Kamati za Maendeleo za Kata, Timu ya Menejimenti (CMT), Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango na Baraza la Madiwani, waliazimia kuanzisha shule mpya 23 za sekondari badala ya kujenga vyumba 267 vya madarasa katika shule 39 zilizopo kutokana na sababu mbalimbali.
Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na kuwa baadhi ya shule hizo tayari zina idadi kubwa ya wanafunzi ambapo yakiendelea kujengwa madarasa zaidi katika shule hizo, bado idadi ya wanafunzi itaendelea kuwa kubwa zaidi suala ambalo linaweza kuleta tena changamoto nyingine ya namna ya kuwaongoza au kuwasimamia wanafunzi hao.
Aidha wanafunzi wengi hutembea umbali mrefu wa kwenda na kurudi shuleni ambapo baadhi hutembea kilomita 20 na zaidi, hivyo kuanzisha shule mpya katika maeneo yao inaweza kuwa msaada kwa wanafunzi hao kwa kupunguziwa umbali wa kwenda na kurudi shuleni lakini pia kuna maeneo ya wazi yanayoruhusu kujenga shule mpya.
Sababu nyingine iliyoangaliwa ni utoro wa muda mrefu kwa wanafunzi unaosababisha pia matokeo hafifu ingawa chanzo kikubwa kikitajwa pia kuwa ni umbali wa kwenda na kurudi shuleni, hivyo kuanzisha shule mpya katika maeneo wanakotoka wanafunzi hao kunatarajiwa kupunguza utoro na kuongeza ufaulu na hamasa ya kusoma kwa wanfunzi wenyewe na jamii kwa ujumla.
Baadhi ya wananchi waliona changamoto hizo mapema na kuchukua hatua za kuanzisha ujenzi wa shule mpya kwa nguvu zao ili kupunguza changamoto hizo, ambapo kwa sasa Halmashauri inaunga mkono juhudi zao kwa kuwapatia fedha za kukamilisha miradi hiyo.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Jemedari Samia Suluhu Hassan imeendelea kuonyesha kujali Sekta ya Elimu kwa kuboresha na kujenga miundombinu hiyo kwa gharama kubwa huku ikitazamia kuwasaidia watoto wa kitanzania kupata Elimu bora katika miundombinu bora pia, ambapo kupitia madarasa ya UVIKO 19 Halmashauri ya Wilaya ya Geita ilipata jumla ya vyumba 352 vya madarasa vinavyotumika kwa sasa kama ilivyokusudiwa.
Hivyo linabaki jukumu la kila mtanzania kujitafakari namna gani anauunga mkono juhudi hizo za Serikali katika kufanikisha hilo na ndio sababu kuu inayowafanya viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wanaendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki katika miradi hiyo kwa kuchangia nguvu zao katika kuchimba msingi, kusogeza mawe, maji na vingine vinavyowezekana kwa sababu ni hulka ya ustaarabu tu, ukifadhiliwa nyama unatafuta chumvi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa