Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Geita ndugu Ali A.Kidwaka amewapongeza wananchi wa kijiji cha Kamena walioamua kujenga vyumba saba vya madarasa kwa nguvu za wananchi ambavyo vitasaidia kutatua changamoto ya madarasa katika shule ya msingi Kamena.
Akiongea na wananchi hao katika shule ya msingi Kamena wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo amewasihi kuendelea kushiriki kutatua baadhi ya changamoto ambazo ziko chini ya uwezo wao kwani kuendelea kuisubiri serikali kufanya kila kitu wanaweza kuchelewesha maendeleo yao.
“Niwapongeze kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya na mnaendelea kuifanya na Tumeona jitihada mnazoendelea nazo na sisi kama Halmashauri tutawapa mifuko thelathini(30) ya saruji katika kushiriki ujenzi huu, Na niwakumbushe ujenzi wa miundombinu ya afya na elimu unaendelea katika kila kijiji na kila kata katika Halmashauri yetu hivyo tumeamua kutoa mabati na mbao za kuezekea kwa wale watakaomaliza ujenzi wa maboma mapema sasa kazi ni kwenu kukimbizana na muda.” Ali Kidwaka.
Aidha Kaimu Afisa Ardhi na Maliasili bwana Faraja B Kaluwa amewataka wananchi wa kijiji hicho kutenga, kuyalinda na kuyahifadhi maeneo yao kwa kuweka mipaka rasmi na kuwatahadharisha kuwa mahitaji ya ardhi yanaendana na wakati hasa katika kipindi hiki ambacho kuna uhitaji mkubwa wa kuongeza miundombinu ya afya na elimu ni vizuri kuwa na maeneo ambayo yamepimwa ili yasivamiwe.
Shule ya Msingi Kamena ina jumla ya wanafunzi 1708 kuanzia darasa la awali mpaka la saba na ina vyumba vya madarasa 10 ikiwa na upungufu wa vyumba ishirini ambapo mpaka sasa ujenzi wa vyumba saba unaosimamiwa na wananchi unaendelea na hii itasaidia katika harakati za kutatua changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa