Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo ametoa wito kwa wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi na usafirishaji kufuata taratibu na sheria zilizowekwa na Serikali kwa lengo la kulinda usalama wa raia na kufanya uvuvi endelevu.
Mhe. Shimo ameyasema hayo Juni 11, 2022 alipoambatana na kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Geita kuzungumza na viongozi, wafanyabiashara, na wananchi wa kijiji cha Ihumilo eneo la Mwalo wa makatani katika kata ya Nkome.
Amewataka viongozi wa mialo yote kusimamia sheria na tahadhari zote kabla ya kuingia majini ikiwemo uvaaji wa maboya ili kudhibiti ajali za majini ambazo hupoteza maisha ya watu ambapo kwa kipindi cha wiki moja kuna watu watatu wamepoteza maisha kwa ajali za majini.
Amewataka pia wavuvi wa mialo yote ukiwemo mwalo wa Makatani kufanya uvuvi endelevu ambao unazingatia kiwango halali cha nyavu zinazotambulika na kuidhinishwa kutumika katika shughuli hizo za uvuvi wa samaki, kuliko kutumia dhana haramu ambazo zinatoa hadi samaki wachanga jambo ambalo ni hatari kwa kuwa linatishia kupotea kwa samaki wakubwa miaka ijayo.
Baada ya kusikiliza kero za wananchi na kuzijibu Mhe. Shimo, amewataka wanachi wote kwa pamoja kuzingatia katazo la kutoonekana watoto wenye umri wa kuwa shule wakifanya kazi katika maeneo hayo, huku akitoa wito wa jamii kuwawezesha kwa chakula mashuleni ili kuongeza ufaulu kwa watoto wao, sambamba na kuhifadhi Misitu na kupanda miti ili kuendeleza uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake Insp. Edward Lukuba Afisa Zimamoto Wilaya ya Geita akiongea na wananchi hao amekumbusha pia kuchukua tahadhari zote kabla ya kuingia kwenye maji kwa kuhakikisha wanakuwa na maboya, Majaketi ya kuzuia kuzama (Life Jackets), na filimbi ambavyo vifaa hivyo vinaweza kuzuia madhara makubwa endapo chombo kitapata ajali.
Insp. Lukuba amewasisitiza pia kubeba mizigo au watu kulingana na mahitaji ya vyombo vya usafiri wanavyotumia kwa kuacha kuzidisha, ili kuepuka ajali za vyombo vya majini zinazosababishwa na uzidishwaji wa mizigo.
Wakati huo huo amesema kuwa kila chombo cha majini kinapaswa kuwa na kifaa cha kuzimia moto (fire extinguisher), na kinasa radi ili kuepuka ajali za moto ndani ya maji ambazo zinaweza kusababishwa na radi kama chombo husika hakijafungwa kifaa maalumu cha kunasa radi.
Sambamba na hayo amewakumbusha wananchi pia kuchukua tahadhari za mioto majumbani kwa kuwa na vifaa vya kuzimia moto (Fire extinguisher), na kuwa na matumizi sahihi ya umeme na majiko ya gesi ambayo yamekuwa yakisababisha ajali za mioto mara kwa mara majumbani huku akisisitiza matumizi sahihi ya majiko ya gesi ikiwa ni pamoja na kubadilisha vifaa ya majiko hayo kwa wakati kama wanavyoshauriwa na wataalamu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa