Na. Michael Kashinde
Kuelekea kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Samwel Shimo ametoa rai kwa watanzania kuanzia ngazi za familia kuhakikisha wanailinda, kuitunza na kuihifadhi Amani ya nchi yetu ili kuendelea kuona mabadiliko katika sekta mbalimbali hapa nchini ikiwemo uchumi.
Ameyasema hayo Disemba 7, 2022 akiwa katika Kata ya Katoro katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita akiongoza zoezi la usafi na kupanda miti katika Kata hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kijamii kuelekea kilele cha maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru wa Tanganayika hapo Disemba 9, 2022.
Mhe. Shimo akizungumza na viongozi na wananchi mbalimbali katika Hospitali yenye hadhi ya Wilaya Katoro pamoja na Kituo cha Afya Katoro, amesema kuwa siri ya mafanikio makubwa yanayoonekana kwa sasa baada ya Uhuru, ni Umoja na Mshikamano uliopo baina ya watanzania na viongozi wao kuanzia awamu ya kwanza hadi sasa awamu ya sita, ambao umechangia kubadilisha hali ya nchi ya Tanzania kimaendeleo na kiuchumi.
DC Shimo amesema kuwa wakati nchi inapata Uhuru wake mwaka 1961 hakukuwa na huduma bora za kijamii kama vile hospitali, barabara na maji kama ilivyo sasa, huku akiwataka watanzania kuendelea kuwapongeza viongozi wa Taifa hili kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ambapo pia amewaasa watanzania kuendelea kuwaunga mkono viongozi wao ili kupata maendeleo Zaidi.
Akiongoza zoezi la usafi wa mazingira na kupanda miti DC Shimo amewataka pia wananchi kuazia majumbani, sehemu binafsi na za wazi kupanda miti ya aina mbalimbali ikiwa ni sehemu ya utunzaji wa mazingira na kudhibiti mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo upandaji huo wa miti ya kutosha unaweza kuwa na faida mbalimbali kama vile lishe bora kwa miti ya matunda, kivuli na faida mbalimbali za kiuchumi huku akiwasisitiza kuitunza vizuri miti hiyo ambayo itakuwa kumbukumbu ya miaka 61 ya Uhuru.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro Bw. Damian Aloyce amesema kuwa mpaka sasa Kuna jumla ya miti 4,000 ambapo katika eneo la Hopitali yenye hadhi ya Wilaya Katoro tayari imepandwa miti 130, huku miti mingine ikiendelea kugawiwa katika Taasisi mbalimbali zikiwemo shule kwa ajili ya zoezi hilo la kupanda miti ikiwa ni sehemu ya shughuli zinazofanyika katika maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika.
Taasisi nyingine zilizopatiwa miti kwa ajili ya kupanda ni pamoja shule ya msingi Mji mwema miti 200, eneo la shule ya sekondari Ludete miti 300, shule ya sekondari Mgunga miti 400, shule ya sekondari Bulengahasi miti 400, na shule ya Sekondari ya Mama Samia ikitarajiwa kupatiwa pia miti 400.
Kaimu Mhifadhi misitu Wilaya ya Geita Sandusy Ngunyale amesema kuwa zoezi la kupanda miti limeanza Disemba 6, 2022 katika vijiji vya Buziba na Bufunda kabla ya kufika Katoro ambapo licha ya kuwashukuru wananchi kwa namna walivyoshiriki katika zoezi hilo ameendelea kuwahamasisha wananchi kuchukua na kupanda miti isiyopungua mitano majumbani.
Aidha Ngunyale ametoa mwongozo kwa watu wanaoishi vijijini kufika katika ofisi za watendaji wa vijiji ili kupatiwa miti ya kwenda kupanda, ambapo pia kwa wakazi wa Geita wanaweza kufika katika kitalu cha Wakala wa Misitu kilichopo Magogo na kupatiwa miti hiyo huku wakihamasishwa kuitunza ili ikue kama inavyotarajiwa.
Picha zaidi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa