Na Michael Kashinde
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo amewataka viongozi na watendaji wa ngazi mbalimbali kuendelea kuihamashisha jamii ili iitikie katika Kampeni ya chanjo ya Polio awamu ya tatu inayoendelea kutolewa katika vituo vyote 53 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.Akiwa katika kikao cha kamati ya Afya Wilaya ya Geita kilichofanyika katika ukumbi wa EPZD Agosti 31, 2022 Mhe. Shimo amewataka wajumbe wa kamati hiyo ya Afya kufikisha Elimu ya chanjo hiyo kwa jamii ili wananchi wajue umuhimu wake, huku akieleza kuwa ana Imani kampeni hiyo itaenda vizuri kama linavyoendelea zoezi la Sensa ya watu na makazi.
Aidha Mhe. Shimo ametumia pia nafasi hiyo kuwataka wajumbe hao wawahamasishe wakulima kujiandikisha ili wapate mbolea ya ruzuku ambayo Serikali imelipa nusu ya gharama ya mbolea hiyo kwa lengo la kumsadia Mkulima kufanya kilimo bora huku akitolea mfano kuwa mkulima ambaye atatambulika ana uwezo wa kununua mbolea inayouzwa Tshs.100,000/= kwa kutoa Tshs.50,000/=
Awali Bw. Jalion Munyi Mratibu wa Chanjo Halmashauri ya Wilaya ya Geita akiwasilisha taarifa ya zoezi hilo kwa awamu zilizopita na mpango kazi wa awamu ijayo, amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita katika mzunguko wa pili uliofanyika kati ya May 18 -21 ilifanikiwa kuchanja watoto 243,210 ambao ni sawa na 123% kutoka watoto 197,695 ambao ndio ilikuwa idadi lengwa. Aidha Bw. Munyi amesema kuwa kwa awamu hii ya tatu kila Halmashauri imepewa lengo la kuwafikia watoto wote walio na umri chini ya miaka mitano ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Geita inatakiwa kuwafikia watoto 250,487 huku changamoto mbalimbali zilizojitokeza awamu zilizopita kama vile uhaba wa vifaa vya kubebea chanjo zikitatuliwa ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Geita mpaka sasa imepokea vifaa hivyo vya kutosha vikiwa 474.
Lengo la Kampeni hii katika mzunguko wa tatu ni kuongeza kinga zaidi mwilini dhidi ya virusi ya Polio ambapo zoezi hili litafanyika nyumba kwa nyumba kwa watoto waote walio na umri chini ya miaka mitano kwa muda wa siku 4 kuanzia 1 Septemba hadi 4 Septemba, 2022 ambapo pia huduma nyingine zitakuwa zikitolewa kama vile elimu ya Chanjo, kuimarisha huduma za chanjo katika vituo vya kutolea Chanjo, na kuwatafuta na kuwafuatilia watoto wote wenye umri chini kumi na tano ambao wamepata ulemavu wa ghafla na kutoa taarifa vituo vya karibu.Kwa mara ya mwisho Tanzania ilipata mgonjwa wa Polio mwezi Julai 1996 ambapo hivi karibuni nchi ya Malawi ilitoa taarifa ya mgonjwa wa Polio mnamo tarehe 17 Februari, 2022 ambapo Tanzania iliamua kuchukua hatua madhubuti ikiwemo kutoa chanjo ya Polio kwa kuwa takwimu zilizofanywa na Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO) zilionesha kuwa nchi yetu ni miongoni mwa nchi zilizo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa Polio.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa