Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo amewapongeza viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ambao wameshiriki kusimamia zoezi la ugawaji wa fedha za Mapango wa TASAF kwa kaya lengwa, huku akitoa rai kwa wanufaika kutumia fedha hizo kwa shughuli za uzalishaji mali ili fedha hizo ziwe na tija kwao.
Mhe. Shimo amezungumza hayo June 6, 2022 alipoambatana na kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Geita kukagua malipo hayo kama walengwa wamepata kiasi halali wanachostahili, ambapo katika ziara yake hiyo ametembelea kata za Bukoli katika kijiji cha Ikina pamoja na kata ya Butobela katika kijiji cha Nyakagwe na kuzungumza na walengwa hao.
Baada ya ukaguzi Mhe. Shimo amewapongeza viongozi waliosimamia zoezi hilo la ugawaji fedha kwa kusimamia vizuri na kutoa kiwango kinachotakiwa kwa walengwa, huku akiwataka wahusika wa mpango huo kutumia fedha hizo kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali kwa kuwa malengo ya viongozi wakuu wa Serikali ni kuona walengwa wanajikwamua kiuchumi kupitia mpango huu.
Aidha Mhe. Shimo ameendelea kutoa wito wa kuwataka wanufaika hao kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu suala litakalowasaidia wao wenyewe kujua taarifa mbalimbali zinazohusu masuala yao ya kifedha na kuepusha mazingira ya kupunjwa au kuibiwa na watu wao wa karibu ambao wakati mwingine wanawatuma kuwapokelea fedha hizo.
Wakisoma risala kwa niaba ya wanufaika wa Mradi huo Bi. Annastazia Andrea Kanama kutoka kijiji cha Ikina na Selemani Kihalo Mang’asa kutoka kijiji cha Nyakagwe wamesema kuwa kupitia fedha hizo wamefanikiwa kupata ada za kuwasomesha watoto na kuanzisha miradi mbalimbali kama vile ufugaji na shughuli za kilimo huku wakimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kupitia mpango huo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa