Oktoba 31,
Maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa yamefanyika katika viwanja va Shule ya Msingi Nzera iliyopo Kata ya Nzera huku lengo kuu la maadhimsho hayo likiwa ni kutoa elimu ya Lishe kwa jamii kwa kuzingatia mapendekezo ya Mwongozo wa Kitaifa wa Chakula na Ulaji (Food Based Diatary Guidelines) ili kuondoa dhana potofu na mitazamo hasi iliyopo inayohusu ulaji na ulishaji wa Watoto katika jamii.
Akizungumza katika maadhmisho hayo, Mkuu wa Wilaya, Geita Mhe. Hashim Komba amezitaka shule kuja na ubunifu ili kuhakikisha zinazalisha chakula cha kutosha ambacho kitakidhi mahitaji ya watoto mashuleni pamoja na kuondokana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na lishe duni.
“Tuje na ubunifu wa kuzalisha chakula kwenye maeneo ya shule. Uwe ni wajibu wa kila kamati mashuleni kuhakikisha tunazalisha chakula cha kutosha mashuleni. Afisa Elimu Msingi pamoja na Sekondari, moja ya EK muhimu kwenye vikao vyetu iwe ni hoja ya kuzalisha chakula mashuleni kwa kutumia maeneo yetu ipasavyo, haswa kipindi hichi cha mvua.” Amesema Mhe. Hashim Komba.
“Tumekwisha waagiza Maafisa Tarafa washirikiane vyema na watendaji wetu wa kata na wa vijiji, kuwaongoza vyema Maafisa Elimu Kata, Walimu Wakuu, kwa kufanya vikao vya wazazi na walezi kwenye shule zetu, ili watoto wapate chakula wawapo shuleni. Hoja ya chakula shuleni ipewe kipaumbele ili tuwasaidie watoto kupata lishe bora na tuondokane na changamoto za utapiamlo na udumavu kwenye jamii yetu.” Ameongeza Mhe Komba.
Mkuu wa Wilaya, Geita Mhe. Hashim Komba ameitaka jamii iondokane na mila potofu pamoja na kuisaidia Serikali kuhakikisha lishe bora inapatikana kwenye maeneo yao.
Aidha, Mhe. Komba pia amewataka wananchi kuhakiksha wanakuwa makini na tabia za ulaji ili kuweza kuzuia magonjwa yanayoweza kujitokeza kutokana na ulaji usiofaa.
“Uhai na Afya ya mwanadamu, siri kubwa ipo kwenye namna anavyokula kwenye maisha yake. Ulaji usiofaa unapelekea magonjwa ya shinkizo la damu na kisukari. Pamoja na sababu nyingine zinazochochea magonjwa haya, lakini mtindo wetu wa ulaji unachangia kwa kiasi kikubwa. Natoa rai tuzingatie lishe bora na kile tunachokula muda wote.” Amesema Mhe. Komba.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Geita Ndg Karia Magaro amewasihi wananchi kutumia vizuri fursa ya ardhi inayowazunguka kupanda mazao tofauti ambayo yatakuwa na tija kwenye suala zima la Lishe bora.
“Jambo la msingi ni kuhakikisha tunatumia vizuri fursa ya ardhi tuliyokua nayo kupanda mazao. Ardhi yetu ni nzuri na hivyo inaruhusu upandaji wa mazao mengi. Hivyo ningependa kushauri tujitahidi kila mmoja wetu katika eneo lake apande walau matunda ili kuboresha afya zetu. Tukiwa na lishe bora tutakuwa tumeimarisha afya za familia zetu na hivyo kuepukana na magonjwa” Amesema Ndg Magaro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Geita Ndg Karia Magaro amewaasa wananchi kutumia fursa ya eneo la ardhi linalowazunguka kupanda mazao yenye tija pamoja na kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuwa na afya bora na kuondokana na magonjwa.
Awali, Afisa Lishe kutoka Halmashauri ya Wilaya, Bi. Umi Kileo, aliainisha changamoto ambazo bado wanakutana nazo kwenye jamii, likiwemo suala la baadhi ya wazazi kutokufuata muongozo sahihi wa ulishaji kwa watoto, muitikio duni kwa baadhi ya wazazi kuchangia chakula kwaajili ya watoto mashuleni, pamoja na kuwepo kwa mila na desturi potofu zinazochochea hali duni ya lishe kwenye jamii.
Aidha, Bi. Umi pia hakusita kuipongeza serikali kwa mchango wake katika utoaji wa elimu kwa jamii kuhusiana na Lishe bora pamoja na kuboresha huduma za afya, haswa kwa kundi la akina mama na watoto.
Afisa Lishe kutoka Halmashauri ya Wilaya, Bi. Umi Kileo amesema elimu bado inahitajika katika jamii kuhusiana na Lishe bora ili kuwa na jamii yenye afya bora.
“Niipongeze Serikali kwa kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii, ikiwemo suala la kuelimisha jamii itambue umuhimu wa kuwapeleka watoto katika vituo vya afya, kwa lengo la kupata chanjo na elimu ya afya na lishe. Pili kuendelea kutoa elimu ya lishe kupitia klabu za afya na lishe mashuleni, na mwisho kuhakikisha inasimamia sheria mbalimbali zilizowekwa ili kuhakikisha haki za watoto zinalindwa.” Amesema Bi. Umi Kileo.
Maadhmisho hayo yaliyokuwa yamebeba kauli mbiu ya, “Mchongo ni Afya yako, Zingatia unachokula,” yamelenga kuhakikisha jamii inazingatia ulaji unaofaa ili kuondokana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na lishe duni.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa