DC ATOA ANGALIZO WATAKAOHUJUMU MRADI WA TASAF
MKUU wa Wilaya ya Geita mkoani hapa, Mwalimu Fadhili Juma amewatahadharisha viongozi wa umma kutojaribu kuhujumu na kukwamisha utekelezwaji wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya Mpango wa Kusaidia Kaya Masikini Nchini (TASAF) kwani watakapobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Mwalimu Fadhili alisema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya utambuzi wa kaya masikini halmashauri ya wilaya ya Geita na kusisitiza atakayerudisha nyuma juhudi za kutokomeza umasikini ofisi yake haitamuonea huruma kwani kila mmoja anatakiwa kuunga mkono mradi huo.
Pia aliwataka viongozi waliochaguliwa kuratibu na kusimamia usajili wa kaya masikini kuendesha zoezi hilo kwa uwazi pasipo udanganyifu ili awamu hii ya mradi iweze kuleta matokeo chanya zaidi na na kufikia adhimio la maendeleo endelevu kwa wilaya ya Geita.
“Huyo mtu ambaye atajaribu kuhujumu mradi, hatutamwacha, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na atapotezwa, atapotezwa kwa maana ya hatakuwa na nafasi kwa wilaya ya Geita kwa sababu hatuna nafasi ya kukaa na mtu ambaye ni mhujumu uchumi.
“Kwa wanufaika wa TASAF naomba waendelee kama nilivyojirizisha hapo awali, hii pesa siyo ya starehe, hii pesa haitakuwa endelevu kwamba miaka yote inakuja, na mpango utafikia mwisho,,, waachane kutumia hizi pesa kwa ajili ya kufanyia sherehe na starehe, wanatakiwa wawekeze miradi ambayo itakuwa endelevu,” alisisitiza.
Mratibu wa malipo ya TASAF kwa njia za kielektroniki, Josephine Joseph akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, alisema kipindi hiki cha mradi usajili na utambuzi wa kaya masikini nchi nzima utafanyika kwa njia ya kielektroniki kwa kutumia vishikwambi, ili kupunguza udanganyifu na uwepo wa kaya hewa uliojitokeza kwa awamu iliyopita.
Mradi ulianza kutekelezwa mwaka 2013 na umeweza kufikia jumla ya kaya milioni moja na laki moja zenye jumla ya walengwa takribani milioni tano sambamba na kuweza kufikia asilimia 70 ya vijiji vyote nchini ambapo kwa kipindi hiki cha pili mradi unatarajia kufikia asilimia 30 iliyobakia na kukamilisha asilimia 100 ya vijiji vyote.
Aidha mradi unatarajiwa kutumia shilingi tillioni 2.03 sawa na asilimia 0.5 ya pato la taifa, ambapo serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania itatoa Shilingi Bilioni 32.2 na kiasi kingine kinatarajiwa kutolewa na wadau wa maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia(WB), serikali ya Norway, Switzerland, Umoja wa Ulaya (EU) na mashirika ya umoja wa mataifa.
“Katika kipindi hiki tunategemea kuongeza walengwa kama laki tatu na kufikia walengwa million 1.45 na walengwa watapokea ruzuku kwa njia ya kielektroniki kupitia simu za mkononi pamoja na akaunti za benki au kwa njia ya mawakala na watatumia namba za NIDA kutambulika,,,, na ruzuku zitakazotolewa ni ruzuku ya msingi, ruzuku ya mashariti na ruzuku ya walemavu,” alifafanua.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa