Baraza maalum la kujadili Mpango na Bajeti limepitisha bajeti ya shilingi bilioni 77.3 kwa mwaka wa fedha 2019/2020, ili kutekeleza mipango pamoja na shughuli mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Geita ikiwemo Miradi ya Maendeleo.
Hata hivyo Baraza hilo limekubaliana kuzigawa fedha za CSR kwa mwaka 2019/2020 zenye jumla ya shilingi Bilioni5, ambapo Bilioni 2.9 zitagawiwa katika kila kata ili kutekeleza miradi ya vipaumbele na fedha zilizobaki kupelekwa kwenye miradi ya huduma pamoja na miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ya Elimu Msingi.
Akizungumza katika Baraza hilo la kujadili Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ali Kidwaka amesema katika mwaka wa fedha uliopita 2018/19, Halmashauri ilijitahidi kukusanya mapato na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kushirikiana na wananchi.
Amesema nguvu za wananchi zilizotumika ni takribani bilioni 3, ambazo zilichangia katika kutekeleza miundombinu ya Elimu pamoja na Afya, hivyo amewashukuru wananchi kwa mchango wao mkubwa walioutoa na kuomba kuendelea kushirikiana katika mwaka 2019/20.
Aidha Mkurugenzi amesema Halmashauri itaendelea kufanya kazi kwa dhati na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ili kuweza kutekeleza shughuli zilizopangwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020.
Mhe. Elisha Kapuga ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilya amewaasa madiwani kuendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuendelea kujitoa kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa