Na: Hendrick Msangi
Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Geita uliofanyika Novemba 15, na 16, 2023 umeutaka Uongozi wa Halmashauri hiyo kuwarudisha kwenye vituo vyao vya kazi Watendaji wa vijiji ambao walihamishwa kwa taratatibu za kiutumishi kwenye vituo vyao vya awali ili wakabidhi ofisi ikiwa ni pamoja na kulipa madeni ambayo wanadaiwa na wananchi wa vijiji hivyo.
Akizungumza kwenye baraza la Madiwani Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mhe Charles Kazungu amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuchukua hatua za kiutumishi kwa kuwaandikia barua watendaji hao ambao wameoyesha kukiuka maadili ya kiutumishi na kuwataka warudishe fedha za wananchi walizochangisha kwa ajili ya miradi katika vijiji vyao.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani
“Niendelee kusisitiza ofisi ya Mkuregenzi kuwaandikia barua Watendaji hao waende kumalizana na wananchi na wasipofanya hivyo kanuni na taratibu za kiutumishi zitumike juu yao tunahitaji watumishi waadilifu” alisema Mhe Kazungu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Cornel Maghembe katika baraza hilo ameelekeza uongozi wa Halmashauri unapofanya mabadiliko kuhakikisha watumishi wanaotoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine wanafanya makabidhiano ya kiofisi na kuhakikisha wanamalizana na wananchi. “Mtakumbuka mwenyekiti wa CCM Mkoa alizungumzia vijiji viwili kwenye kata ya Nkome ambayo kuna mtendaji amehamishiwa kwenda kijiji kingine na inasemekana ameondoka na milioni 10 za wananchi “alisema Maghembe
Aidha aliwataka watendaji ambao wamehamishwa wakaripoti kwenye ofisi walizopangiwa na badaye warudi kwenye vijiji vyao kumalizana na wananchi.
Pamoja na hayo Mheshiwa Faraji Seif amabaye ni Diwani wa kata ya Bukoli ambao watendaji wa vijiji hivyo vya Ntono na Ikina wanakotoka amesema anakiri kuwepo kwa madeni hayo kutoka kwa wananchi ambao amesema iwapo zitafanyiwa uchunguzi zitakuwa ni zaidi ya hizo ambazo wananchi wanalalamika kuchangishwa na hazikupelekwa benki au kufanya kazi iliyokusudiwa.
Kwa upande wa uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Geita umesema umeliopokea jambo hilo na litafanyiwa kazi kwa uharaka kwa kuchukua hatua stahiki.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa