BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita leo May 8,2024 katika Kikao chake cha kawaida, limewasilisha taarifa za utekelezaji wa Shughuli za Serikali ngazi ya kata kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2024.
Jumla ya Kata 37 zimewasilisha taarifa katika baraza hilo ambapo Waheshimiwa Madiwani wameeleza changamoto mbalimbali zinazozikabili kata hizo zikiwepo za kuharibika kwa miundombinu ya barabara zinazounganisha maeneo mbalimbali kunapopelekea magari kushindwa kupita ikiwa ni pamoja na uharibifu wa miundombinu ya madarasa kutokana na mvua kubwa zenye upepo mkali zinazoendelea kunyesha.
Aidha Madiwani hao katika uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa Shughuli za Serikali ngazi ya kata wameeleza changamoto ya uhaba wa walimu wa kike katika Shule nyingi na kuitaka ofisi ya Mkurugenzi kuendelea kufanya msawazo wa walimu wa kike ili kumaliza changamoto hiyo.
Pamoja na hayo, Waheshimiwa Madiwani wamesema kuchelewa kwa ukamilishwaji wa Miradi ya Maendeleo ambayo kampuni ya GGML inaietekeleza kunatokana na vifaa vya ujenzi kutokufika site kwa wakati na kupelekea mafundi kukaa site bila kazi.
Akizungumza katika Baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Charles Mabeyo Kazungu ameilekeza ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kuwaita wasimamizi wa Miradi kutoka kampuni ya GGML kushiriki vikao vya Baraza la Madiwani ili waweze kuzisikiliza changamoto zinazowasilishwa na Waheshimiwa Madiwani.
Aidha Mhe Kazungu ameiomba Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuingilia kati Miradi inayotekelezwa na mfuko wa CSR kutoka GGML ili kuharakisha ukamilishwaji wa Miradi viporo ikiwepo maboma yaliyo jengwa kwa nguvu za Wananchi.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nyamilolelwa Mhe Mashauri Gambula amesema mapato mengi ya Halmashauri yanapotea kufuatia ubovu wa barabara hasa barabara ya Saragulwa - Mgusu kukatika na kupelekea kikwazo katika Shughuli za uchumi kwa wananchi wa kata zote mbili na nje ya Halmashauri.
Akifunga kikao cha Baraza hilo kwa siku ya kwanza, Mhe Kazungu amewashukuru Waheshimiwa Madiwani kwa uwasilishaji mzuri wa Shughuli za Serikali ambazo zinatekelezwa kwenye kata zao, na kuwataka kuendelea kutatua changamoto ambazo zipo kwenye kata zao huku wakiwashirikisha Wananchi na wadau mbalimbali ili kuendelea kukabiliana na changamoto.
Pamoja na hayo amewataka Waheshimiwa Madiwani kuendelea kuwaelimisha wananchi katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuwataka kuwa wavumilivu kwani Serikali ipo kazini, kurekebisha miundombinu iliyo haribiwa na mvua kubwa zilizokuwa zikiambatana na upepo mkali.
"Muwaambie Wananchi kuwa na tahadhari kutokana na mabadiliko ya Hali ya hewa yanayotokea kutokana na mvua na upepo mkali ili wawe salama." Amesema Mhe Kazungu.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wakuu wa Idara na vitengo kutoka Halmashauri ya wilaya ya Geita, Viongozi wa Chama na Serikali . Baraza hilo litaendelea siku ya tarehe 9, May 2024.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa