Nzera-Geita
Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita leo Machi 10, 2025 katika kikao chake kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri-Nzera na kuongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe Hadija Said ,Limeridhia Pendekezo la kuanzisha Jimbo jipya katika Tarafa ya Butundwe.
Waheshimiwa Madiwani wakiwa Katika Mkutano wa Baraza Maalum la Madiwani kujadili Pendekezo la Kuanzisha Jimbo Katika Tarafa ya Butundwe
Halmashauri ya Wilaya ya Geita ni moja kati ya mbili zilizopo ndani ya Wilaya ya Geita, Ikiwa na majimbo mawili ya uchaguzi,Tarafa nne, Kata 37,Vijiji 145 na Vitongoji 593 huku ikiwa na eneo la Kilometa za mraba 5,159.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Hadija Said akiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Dkt Modest Burchad katika Mkutano wa Baraza Maalum la Madiwani kujadili Pendekezo la Kuanzisha Jimbo jipya.
Madiwani hao wameridhia kupitisha pendekezo hilo la uanzishwaji wa jimbo jipya la Butundwe ambapo kutasaidia kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na maendeleo ya kiuchumi ya kisekta na kuimarisha uwakilishi wa wananchi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waheshimiwa Madiwani wakiwa Katika Baraza Maalum Kujadili Pendekezo la Kuanzisha Jimbo jipya katika Tarafa ya Butundwe Machi 10,2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri-Nzera-Geita
Aidha Katika Baraza hilo, Waheshimiwa Madiwani wamepitia malengo mahsusi ya kuanzisha Jimbo ambayo ni pamoja na kupunguza mzigo wa kiutawala kwa jimbo la Busanda na kuboresha utoaji wa huduma za umma, kuwezesha ugawaji wa rasilimali na bajeti kwa ufanisi zaidi kwa kuzingatia mahitaji ya jimbo la Butundwe.
Pamoja na hayo pendekezo la kuanzisha jimbo la Butundwe kutapelekea usimamizi wa miradi ya maendeleo na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Butundwe ambapo tarafa hiyo ina jumla ya kata 11 huku Tarafa ya Busanda nayo ikiwa na kata 11.
Afisa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Bahati Kidaha akiwasilisha pendekezo la kuanzisha jimbo jipya la Butundwe kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji katika Mkutano wa Baraza Maalum.
Kwa Mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Tarafa ya Butundwe ina wakazi 377,189 ambapo kwa kutumia wastani wa ongezeko la idadi ya watu wa asilimia 5.4 kwa mwaka hadi kufikia 2025 tarafa ya Butundwe inakadiriwa kuwa na idadi ya watu 443,527 ambapo kwa mujibu wa kanuni ya Tume huru ya Uchaguzi na 18(3) kwa majimbo ya vijijini ili kuanzisha jimbo jipya inatakiwa idadi ya watu kuanzia 400,000.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa