Na: Hendrick Msangi
WATENDAJI wa Kata na Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wametakiwa kuweka fedha benki kwa wakati baada ya kukusanya tozo mbalimbali kama mapato ya Halmashauri kufuatia kuwepo kwa tabia ya watendaji hao kukaa na fedha za serikali kwa muda mrefu bila kuziweka benki.
Maelekezo hayo yametolewa Machi 13, 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambapo kilifanyika kikao elekezi kwa watendaji hao na timu ya menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Watendaji wa Kata na Vijiji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakiwa kwenye kikao ndani ya ukumbi wa Halmashauri ambapo kwa pamoja waliazimia kuweka fedha za mapato ya halmashauri ndani ya masaa 24 baada ya kukusanya katika vyanzo mbalimbali vya mapato kupitia mashine za kukusanyia ushuru (POS)
Wakizungumza kwa nyakati tofauti juu ya sababu zinazopelekea kutokuweka fedha za serikali kwa wakati na badala yake kukaa nazo muda mrefu hali ambayo inaipa Halmashauri sifa mbaya, watendaji hao wamesema changamoto kubwa ni kutoka kwa Mawakala kushindwa kufanya miamala hiyo kwa madai malipo ya kutumia control number hayawapi faida katika huduma wanazozitoa, baadhi ya maeneo kuwa na miundombinu isiyokuwa rafiki kuweka fedha ndani ya masaa 24 baada ya ukusanyaji.
Aidha changamoto nyingine zilizotajwa na watendaji hao ni ya kimfumo ambapo miamala inayojirudia kutoa stakabadhi kuchelewa kufutwa kwenye mfumo na wakati mwingine kutokusomeka kwenye mfumo kwa miamala inayolipwa kwa wakati huku changamoto nyingine ambayo ilibaina kwenye kikao elekezi hicho ni baadhi ya watendaji hao kuingia mikataba na vijana ambao huwasaidia katika zoezi zima la ukusanyaji wa mapato jambo ambalo limekuwa likiwaletea usumbufu pale ambapo wanatakiwa kuweka fedha benki na vijana hao kuchelewa kufanya kwa wakati.
Kikao hicho kilifikia maazimio ya pamoja kwamba fedha ya serikali inapaswa kuwekwa benki ndani ya masaa 24 baada ya makusanyo ya tozo mbalimbali katika vyanzo vya mapato vilivyopo kwenye mashine za kukusanyia mapato (POS). “Tumeazimia fedha zipelekwe benki ndani ya masaa 24 na iwapo muda huo hautazingatiwa sheria itachukua mkondo wake kwa kuwawajibisha watendaji wote watakaoshindwa kufanya hivyo na iwapo atakuwepo ambaye ana changamoto ya kushindwa kufanya hivyo awasiliane na Mwasibu wa Mapato kwa wakati” Alisema Bi Sarah Yohana akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji katika kikao hicho.
Pamoja na swala la kuweka fedha benki kwa wakati, watendaji hao waliaswa kuwa waadilifu katika maeneo yao ya kazi ikiwa ni pamoja na kukata ushuru unaostahili kulingana na chanzo husika ambapo kwa wafanyabiashara wanaobeba bidhaa za mazao ya kilimo liliwekwa azimio la kukemea ubebaji wa rumbesa na iwapo mfanyabiashara atakutwa amebeba mzigo kwa kiwango cha rumbesa basi atozwe faini ili kukemea hali hiyo.
Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakifuatilia kikao elekezi kwa watendaji wa kata na vijiji ambapo maelekezo mbalimbali yalitolewa kwa watendaji hao ili kuendelea kuleta sifa njema kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Watendaji hao waliomba uongozi wa Halmashauri uangalie kata ambazo huduma za kifedha sio rafiki kuongezewa muda wa kupeleka fedha benki. “Hatupendi kukaa na fedha za serikali muda mrefu ila wakati mwingine changamoto ya uapatikanaji wa urahisi wa kuweka fedha inayokusanywa husababisha kuchelewesha kuweka fedha” alisema Martine Matiba mtendaji wa kata ya Ludete.
Aidha waliomba kupewa ushirikiano na watumishi wa Halmashauri pale wanapokamata magari ambayo yamebeba mazao bila kulipa ushuru stahiki. “Tunaomba tuaminike baada ya kupewa posi na sio kupewa maelekezo na baadhi ya wakuu wa idara kwa kuwakataza watendaji kukamata magari ya wanasiasa jambo ambalo ni changomoto na linawavunja moyo ikiwa ni pamoja na asilimia 10 itoke kwa wakati ili kusaidia watendaji kutekeleza majukumu yao kwa wakati” alisema Alfred Conrad mtendaji wa kata ya Izumacheri.
Timu ya Kikosi Kazi (Task Force) Ikiwa katika utekelezaji wa ukusanyaji wa mapato ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Wafanyabiashara wamekuwa wakitumia usafiri wa bodaboda na maguta kusafirisha mazao kukwepa ushuru.
Kuhusu Kikosi Kazi (Task Force) kilichoundwa na timu ya menejimenti kwa ajili ya zoezi la ukusanyaji wa mapato, watendaji hao waliomba kuwepo kwa mahusiano mazuri kati yao na kikosi kazi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa pindi Kikosi kazi kinapotembelea kwenye kata kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato ambapo uongozi wa kata utasaidia upatikanaji wa mgambo pale inapohitajika kufanya hivyo katika zoezi zima la ukusunyaji wa mapato.
Naye mwenyekiti wa Watendaji wa Kata ndugu Lusekelo Mwaikenda kwa niaba ya watendaji aliushukuru uongozi wa Halmashauri kwa kufanya kikao na watendaji na kuomba kuendelea kuwepo kwa ushirikiano kati ya watendaji na watumishi ili kuendelea kuinua mapato ya Halmashauri na kuahidi yote waliyo elekezwa kuyafanyia kazi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa