Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba, Oktoba 31,2024 amewataka wananchi Wilayani Geita kuzingatia Lishe bora katika maisha yao ya kila siku.
Wito huo umetolewa katika Kata ya Nzera yalipo Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambapo maadhimisho ya kilele cha siku ya Lishe yenye kauli mbiu “Mchongo ni Afya yako, Zingatia unachokula" yamefanyika.
Akizungumza na wananchi waliojotokeza katika maadhimisho hayo, Mhe Komba amewataka wazazi na wananchi kujenga tabia ya kutafuta na kutumia huduma za Lishe zinazopatikana kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
“Tujenge utamaduni wa kwenda kliniki pamoja akina baba na akina mama ili kupima afya kwa pamoja kwani itawapa faida za kupata elimu kusaidia makuzi ya watoto” amesisitiza Mhe Komba.
Mhe Hashim Komba amewataka akina baba kujenga desturi ya kuongozana na akina mama kwenda kliniki mara kwa mara.
Vilevile Mkuu wa Wilaya amezitaka familia kuzingatia mlo kamili kwa kuzingatia wanachokula kwa kufuata mchanganyiko kutoka makundi 6 ya vyakula ili kuepuka magonjwa kama shinikizo la damu, kisukari, changamoto kwenye figo yanayoweza kusababishwa na mtindo wa ulaji mbovu wa lishe.
“Ukikosea kula vizuri ukala kwa kujaza tumbo yapo madhara utayapata ya magonjwa ambayo hukaribisha umasikini katika kuwahudumia wagonjwa hao , rai yangu tuitumie siku ya lishe kupata elimu kwa namna ambavyo tutakula katika maisha yetu. Ukiwa na Lishe bora umeimarisha afya za familia” amesema Mh Komba.
Aidha Mh Komba ameitaka Halmashauri kupitia idara ya afya, ustawi wa jamii na lishe kwa kushirikiana na idara mtambuka, wadau wa maendeleo na wananchi wote kuhakikisha elimu ya lishe inatolewa kuanzia ngazi ya kaya ili kuendelea kupambana na changamoto za udumavu na utapiamlo.
Kwa upande wake Afisa Lishe (W) Bi Ummy Kileo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kutoa elimu kwa jamii kuhusu afua za lishe.
Maadhimisho ya kilele cha lishe hufanyika kila ifikapo tarehe ya mwisho wa mwezi wa kumi kila mwaka ambapo yameenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Afrika ya usalama wa chakula na lishe (Africa Day for Food and Nutrition Security-ADFNS).
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa