Nkome-Geita
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Rajab Magaro, Aprili 11,2025 ametembelea mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika kijiji cha Mnyala Kilichopo Kata ya Nkome Geita.
Mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ulianza Julai 2024 ukiwa ni mradi wa kikundi cha wajasiliamali Mnyala mchangani ambao umewezeshwa na Serikali ya awamu ya Sita kupitia Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB)
Akizungumza katika Ziara ya kuangalia Maendeleo ya Mradi huo wenye thamani ya Shilingi Milioni 117.5, Mkurugenzi Mtendaji Ndg Magaro amewataka wajasiliamali hao kuendelea kuusimamia mradi huo ili uzalishaji uendelee na kuweza kuendesha familia zao kwa kuwa mahitaji ya samaki ni makubwa.
Pamoja na hayo Ndg Magaro ameiagiza Idara Kilimo na Uvuvi Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuwasaidia wajasiliamali hao namna bora ya kuandaa bwawa kwa ajili ya uzalishaji wa vifaranga vya samaki na kuongeza kuwa Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani ambapo imetenga zaidi ya Bilioni 1.2 kwa ajili ya kukopesha vikundi itaendelea kuwawezesha wajasiliamali ili kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Mratibu kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bi Glacia Marugujo amekipongeza kikundi hicho kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na kusema Benki hiyo itaendelea kutoa ushirikiano kwa kikundi hicho ikiwa ni Juhudi za Serikali ya awamu ya Sita kuwainua wananchi kiuchumi.
Naye Mwenyekiti wa Kikundi hicho Bw.Charles Oruwa ameiomba Halmashauri kuendelea kuwasaidia kupata masoko ya samaki na kuongeza vizimba kwani kwa sasa Kikundi hicho kina vizimba vinne.
" Tunashukuru ofisi ya Mkurugenzi kupitia Wataalam wake Maafisa Uvuvi kwa namna wanavyotuma Ushirikiano wa karibu katika ufugaji wa samaki" Amesema Bw Oruwa Mwenyekiti wa Kikundi hicho.
Aidha Wanakikundi hao wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwawezesha kiuchumi ambapo kwa sasa wanaweza kuendesha shughuli mbalimbali pasipo kutegemea Uvuvi wa kwenye ziwa ambao wakati mwingine upatikanaji wa samaki ni wa shida.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa