Na Michael Kashinde
Katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika maendeleo ya Sekta ya Elimu Shirika la Plan International limetoa vitabu 52,683, vifaa vya michezo pamoja na vifaa vya kujifunzia kwa watoto wenye ulemavu kupitia mradi wake wa miaka 5 wa kuwawezesha wasichana rika balehe kuendelea na masomo (Keeping Adolescent Girls in School - KAGIS) katika mkoa wa Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela akizungumza katika hafla fupi ya kupokea vitabu hivyo Agosti 30, 2022 katika viwanja vya shule ya msingi Mkoani amelishukuru Shirika hilo kwa mchango wake katika maendeleo ya sekta ya Elimu na kwa kutekeleza malengo ya Milenia ya kumpatia elimu mtoto wa kike huku akisisitiza kuwa ukimwelimisha mwanamke umeielimisha jamii kwa kuwa mwanamke ni mchumi namba moja anapowezeshwa.
Mhe. Shigela ametoa wito wa kutumia vitabu hivyo kwa usahihi ili malengo yaliyotarajiwa yafikiwe huku akiishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia kwa kuongeza bajeti ya Elimu bila malipo sambamba kuleta kiasi cha Tshs. 470,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya kila jimbo kupitia mradi wa SEQUIP huku akiendelea kupiga marufuku kuzuia watoto kwenda shule kwa sababu ya kudaiwa michango mbalimbali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo amelipongeza shirika hilo la Plan International kwa kuyajali makundi maalumu katika jamii wakiwemo watoto na watu wenye ulemavu sambamba na kuzisaidia sekta za Elimu, Afya na michezo huku akieleza kuwa Serikali inautambua mchango wao katika kujali na kuboresha mazingira na miundombinu ya watumishi na wanafunzi mbalimbali.
Awali Bw. Nicodemas Gachu ambaye ni Mkurugenzi wa mradi wa KAGIS akitoa taarifa kwa Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigella amesema kuwa mradi huo umelenga kushughulikia changamoto zinazozuia wasichana walio katika umri wa balehe kutambua haki yao ya Elimu salama, bora na inayozingatia jinsia.
Bw. Gachu ameendelea kwa kusema kuwa mradi unatekeleza ajenda ya kitaifa ya kuwekeza katika Afya na maendeleo ya vijana balehe kwa kulenga nguzo nne ambazo ni kutokomeza mimba za utotoni, kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI, kuzuia ukatili wa kimwili, kingono, na kisaikolojia pamoja na kuhakikisha watoto wa Kike na Kiume wanabaki shuleni.
Aidha ameendelea kufafanua kuwa Shirika la Plan International kwa kushirikiana na Serikali ya Canada chini ya mradi wa KAGIS limetoa vifaa hivyo ili kuisaidia sekta ya Elimu ambayo imekuwa na changamoto mbalimbali kama vile upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na umbali kutoka nyumbani hadi shuleni hasa kwa shule za Sekondari. Loyce Andrea Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mkoani amesema kuwa wanashukuru sana kwa kupata vitabu hivyo ambavyo vitawasaidia kujisomea wakiwa shuleni na hata majumbani huku akieleza kuwa wanaweza kufaulu vizuri kwa kusoma vitabu hivyo kwa kuwa mara zote majibu ya maswali mbalimbali yanayotolewa katika mitihani yao yanapatikana katika vitabu hivyo yakiwa na ufafanuzi wa kutosha.
Kupitia mradi huu wa KAGIS chini ya ufadhili wa Serikali ya Canada shirika hilo linampango wa kujenga vyoo 50 katika shule za mradi katika mikoa ya Geita na Kigoma huku baiskeli 2,200 zikisambazwa kwa watoto wa kike wanaolazimika kutembea umbali mrefu kwenda shule sambamba na kutoa Elimu ya Afya ya uzazi na usawa wa kijinsia.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa