Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba, ameanza ziara yake katika Tarafa ya Butundwe leo Machi 11, 2025, akiongozana na viongozi na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza changamoto za wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kata ya Butundwe.
Katika ziara hiyo, Mhe. Komba ametembelea miradi ya afya, elimu na miundombinu, ikiwemo ujenzi wa Zahanati ya Nyandago, Zahanati ya Lukumbo, nyumba za walimu katika Shule ya Msingi Lukumbo na Jengo la Mama na Mtoto katika Zahanati ya Kasangwa. Ameelekeza miradi hiyo ikamilishwe kwa wakati ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Aidha, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Butundwe, Mhe. Komba amesisitiza ushirikiano wa jamii katika kulinda usalama, akihimiza dhana ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi. Pia, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kusajili au kurekebisha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mkuu wa Wilaya ameonya dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watoto wa kike na kuwataka wazazi kuhakikisha wanapata elimu bila vikwazo. “Mtoto wa kike atalindwa, atapewa elimu na hatokatishwa ndoto zake,” amesisitiza.
Kwa upande wa miundombinu, Mhandisi wa TARURA Wilaya ya Geita, Saimon Buganga, amesema zaidi ya Shilingi bilioni 1 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara, huku milioni 491 zikielekezwa kwenye ujenzi wa Barabara ya Chemamba-Kasamwa-Nyandago yenye urefu wa kilomita 18.
Miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa na wananchi ni uhaba wa maji, mmomonyoko wa maadili, migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, pamoja na uwepo wa wanyamapori hatarishi. Mhe. Komba ameahidi kushughulikia changamoto hizo kwa kushirikiana na mamlaka husika.
Ziara hiyo inaendelea kesho kwa ukaguzi wa miradi mingine katika maeneo tofauti ya Tarafa ya Butundwe.
Matukio kwa picha ziara ya Mkuu wa Wilaya katika Kata ya Butundwe
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa