Mikoa 7 ya Tanzania imetakiwa kuchukua hatua za kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaofanywa kwenye mikoa hiyo ili kurudisha uoto wa asili uliopotea.
Ndg Karia Rajabu Magaro, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya Geita, akifyeka nyasi wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani, yaliyofanyika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato Leo Juni Mosi, 2024.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa wito huo kwa mikoa hiyo wakati akiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato sehemu lilipofanyika zoezi la kupanda miti pamoja na kufanya usafi wa mazingira Kimkoa ikiwa ni kuelekea siku ya mazingira duniani.
Mhandisi Cyprian Luhemeja, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, wa pili kushoto aliyevaa shati la maua maua akiwa amesimimama pamoja na Mkuu wa Mkoa Geita Mhe Martine Shigela aliyesimama katikti aliyevaa track suti na kofia nyeusi pamoja na viongozi wengine, wakijiandaa kuhutubia wananchi kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani Leo Juni mosi, 2024.
Mhandisi Luhemeja ametaja mikoa inayotakiwa kuchukua hatua za kukabiliana na uharibifu wa mazingira ili kurudisha uoto wa asili uliopotea ni pamoja na Mwanza, Simiyu, Geita, Shinyanga, Tabora,Singida na Kigoma.
Mhandisi Luhemeja amesema kuwa kama mikoa hiyo haitachukua hatua ya kukabiliana na suala hilo kuna athari kubwa ya mazingira itakayopatikana kwa vizazi vijavyo.
“Kama hatutafanya jambo lolote sasa, miaka 20 ijayo watoto wetu watanung’unika sana, na tusidanganyane na maji ya ziwa Victoria pamoja na kuwa yapo jirani, kuyasambaza ni kazi ngumu sana.
Nilipokuwa Wizara ya maji nilitembelea wilayani Bukombe, pale Bukombe nilikuta hata kuchimba maji ya chini ni shughuli maji yapo mbali sana, lakini hii ni kutokana na kuharibu mazingira hivyo tuanze mipango ya kuanza kuandika miradi ya kurudisha uoto wa asili hali siyo nzuri ’’ameongeza Luhemeja.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela akizungumza kwa niaba ya Mgeni rasmi ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kasimu Majaliwa Majaliwa (MB) amewataka wananchi wanaoshughulika na uchimbaji wa madini kurejesha uoto wa asili kwenye maeneo wanayofanyia kazi zao mara tu wanapomaliza shughuli za uchimbaji.
Viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Geita Mhe Martine Shigela katika zoezi la kufanya usafi wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani yaliyofanyika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato Juni Mosi, 2024.
Aidha amewataka Wananchi wote kuendelea kuona zoezi la kuyatunza mazingira kuwa endelevu kuanzia maeneo wanayoishi na sio jambo la siku moja tuu.
Wakati huo huo Mbunge wa Jimbo la Chato Mhe Medard Kalemani amesema kuwa wananchi wa Chato wataendelea kushirikiana na serikali ili kutunza mazingira kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Mbunge wa jimbo la Chato Mhe Dkt Medard Kalemani aliyevaa shati jeupe, akipunga mkono wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani yaliyofanyika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato Juni Mosi 2024
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Watumishi wa umma kutoka Wilaya za Mkoa wa Geita, Viongozi wa dini, vyama vya siasa na wananchi mkoani Geita.
Kila ifikapo June 5 ya kila mwaka dunia huadhimisha siku ya mazingira duniani lengo likiwa ni kuhamasisha jamii kuelewa masuala ya mazingira na kuifanya jamii kuwa mstari wa mbele kuchukua hatua za kuhifadhi na kulinda mazingira.
Kauli mbiu ya mwaka huu katika wiki ya Mazingira Kitaifa na Kimataifa inasema "urejeshwaji wa ardhi iliyo haribiwa na ustahimilivu wa hali ya jangwa na ukame."
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa