Mbeya-Tanzania
MKUTANO wa 109 wa washitiri wa vipindi vya Elimu kwa umma unaofanyika Katika Ukumbi wa City Park Jijini Mbeya umeanza leo Februari 17 na unatarajiwa kuhitimishwa Februari 21, 2025.
Awali akizungumzia mada ya Maafisa Habari na Uchaguzi katika Mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt Ayub Rioba Chacha amewaeleza washitiri juu ya umuhimu (athari za taarifa/Mawasiliano kwa umoja na usalama wa Taifa na wajibu wa washitiri katika kueleza mafanikio ya serikali.
Dkt Rioba amesema ipo haja ya Maafisa Habari kufahamu namna ambavyo wanaweza kuwasilisha taarifa kwa wananchi wa ngazi zote kuhusu mafanikio ya serikali ili wananchi waweze kuelewa taarifa hizo hasa kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.
"Maafisa Habari mnao wajibu wa kutoa Taarifa zinazogusa au kukidhi mahitaji ya jamii katika ngazi zote ili kuleta athari chanya katika jamii" Amesema Dkt Rioba.
Aidha Dkt Rioba amesema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu , umoja wa Taifa ni muhimu sana katika kulinda misingi na tunu za Taifa kwa maslahi ya Taifa la Tanzania ili Nchi iendelee kuwa salama.
" Tunalojukumu kubwa la Kuisadia nchi yetu kwa kutumia taaluma na utaalam tulio nao kuwaeleza wananchi mambo makubwa na mazuri ambayo yamefanywa na Serikali" Ameongeza Dkt Rioba.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt Venance Mwasse amewataka washitiri wote kuitumia fursa katika Mkutano huo kwa kujifunza kwani Muktadha wa Serikali inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuendeleza umoja na amani.
"Unapotoa taarifa iwe ya kueleweka ili kuepuka kuleta tafrani katika jamii hivyo tunao wajibu wa kuhakikisha taarifa zinaeleweka ili kuleta athari chanya katika jamii" Amesema Dk Venance Mwasse.
Vilevile Dkt Mwasse amesema umma unaopelekewa taarifa umebadilika hivyo maafisa habari watoe taarifa kwa kuendana na Teknolojia inavyobadilika.
Pamoja na hayo, mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwa ni pamoja na vijana na uhifadhi wa mazingira, maendeleo binafsi na matumizi bora ya rasilimali na matumizi ya nishati safi.
Mkutano huo umebeba kauli mbiu isemayo : Tumia Nishati Safi , Tunza Mazingira na utafanyika kwa siku tano ambapo Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Limekuwa likiandaa mafunzo hayo kila mwaka na huo ukiwa ni Mkutano wake wa 109 ambapo wakuu wa Taasisi mbalimbali, maafisa habari na mahusiano kutoka Serikalini wanashiriki.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa