Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Mh. Charles Kazungu, amewataka Wazazi Wilayani Geita kuhakikisha wanawaandikisha watoto wao waliofanikiwa kuchaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza kwa mwaka wa 2025 katika shule ambazo zinaendelea kujengwa katika Wilaya ya Geita.
Akizungumza hii leo kwenye Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Madiwani kwa kipindi cha Robo ya Pili 2024/2025 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya, Mh. Kazungu ametoa maelekezo kwa madiwani kuweka msisitizo kwa wazazi kuhakikisha wanaipa Elimu kipaumbele badala ya kuwatelekeza watoto wakizagaa mitaani.
"Sisi kama madiwani tuna jukumu la kuwahamasisha wazazi wawapeleke watoto shuleni kidato cha kwanza. Hii itasaidia kuondokana na tatizo la kukithiri kwa watoto waliopo mitaani." Amesema Mh. Kazungu.
Jumla ya wanafunzi 13,515 waliofaulu mtihani wa kumaliza Elimu Msingi mwaka 2024, wameweza kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Kwa mwaka 2025, huku 95 kati yao walochaguliwa kwenda shule za Bweni.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Geita, Mh. Charles Kazungu amewataka Madiwani kuwahimiza Wazazi kuwapeleka shule watoto waliofanikiwa kujiunga na Kidato cha Kwanza.
Aidha, Halmashauri kupitia Divisheni ya Elimu Sekondari imeweza kufanya maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa Kidato cha Kwanza kwa kuainisha mahitaji ya vyumba vya madarasa 293, pamoja na viti na meza 13,420.
Kwenye mkutano huo ulioingia siku ya pili, kamati zilizowasilisha taarifa ni pamoja na Kamati ya Fedha, Kamati ya Uongozi na Mipango, Kamati ya Uchumi, Kamati ya Ujenzi na Mazingira, Kamati ya Elimu, Afya na Maji, Kamati ya kudhibiti UKIMWI, pamoja na Kamati ya Maadili.
Hali ya Ukusanyaji wa Mapato na Matumizi wa Halmashauri.
Hadi kufikia mwezi Disemba 2024, Halmashauri imeweza kukusanya kiasi cha Shillingi 520,508,095.24 na hivyo kufanikiwa kuvuka lengo la makisio iliyojiwekea.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Ndg. Karia Magaro ameweza kuipongoze timu ya mapato na kuishauri kuongeza bidii kwenye kasma ambazo bado hazijafikiwa, huku pia akitoa rai kwa madiwani kuweza kuendelea kuisimamia miradi ya kimaendeleo na yenye tija kwa wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndg. Karia Magaro amesema kasi inatakiwa kuongezeka kwenye ukusanyaji wa Mapato ili kuhakikisha Halmashauri inafikia malengo iliyojiwekea.
Maelekezo ya Mkuu wa Wilaya kwa Halmashauri.
Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Geita, Ndg. Hashim Komba, Katibu Tawala wa Wilaya, Bi Lucy Beda amesema kuwa fedha kiasi cha Shilingi 100,000,000 zilizokuwa zimetengwa kwaajili ya miundombinu ya viti na meza, ziwezeze kutolewa kwa haraka kwakuwa shule zimeshafunguliwa.
Katibu Tawala wa Wilaya, Geita, Bi. Lucy Beda ameiagizia Halmashauri kuhakikisha inatoa fedha ili kuwezesha utoaji wa meza na madawati mashuleni.
Bi. Lucy Beda pia hakusita kutoa pongezi kwa Halmashauri kupitia kwa Mkurugenzi kwa kuweza kusimamia utoaji wa mikopo kiasi cha Shilingi 689,000,000 kwa vikundi vya Wanawake, Walemavu na Vijana ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuwataka Madiwani kuwahamasisha Vijana kwa kuchangamkia fursa hiyo.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Geita, Mhandisi Sande Batakanwa akichagia hoja ya Madiwani juu ya ufikishaji wa huduma ya maji karibu na wananchi, zoezi ambalo lipo katika hatua za mwisho kukamilika.
Meneja wa TARURA, Mhandisi Jerry Mwakapemba akiwasilisha mada kuhusiana na uendelezwaji wa ujenzi wa barabara mbalimbali katika Wilaya ya Geita.
Wenyeviti wa Kamati tofauti za Halmashauri wakiwasilisha taarifa za bajeti za Kamati wanazozisimamia kwa kipindi cha Robo ya Pili ya mwaka wa Fedha 2024/2025.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa