Na Hendrick Msangi
KAMATI ya Siasa Wilayani Geita Januari 22 na 23 imefanya Ziara kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita na kuridhishwa na hatua za utekelezaji zilizofikiwa.
Akiongoza kamati hiyo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Geita Komredi Barnabas Mapande ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa usimamizi mzuri wa miradi inayoendelea na ile iliyokamilika.
Akikagua mradi wa nyumba ya mtumishi 2 in 1 katika shule ya sekondari Nzera ambapo ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 99 na kugharimu jumla ya kiasi cha Shilingi 100,000,000 Mwenyekiti huyo pamoja na kamati yake waliridhishwa na hatua za ukamilishwaji wa mradi huo na kulitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufikisha umeme kwa wakati katika jengo hilo. “Kazi ni nzuri, kazi imesimamiwa kwa viwango vyote na hii inathibitisha pasipo shaka dhamira na malengo ya Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuleta fedha nyingi zisimamiwe na zimesimamiwa vizuri.” Alisema Komredi Mapande.
Nyumba ya mtumishi 2 in1 katika shule ya sekondari Nzera ambapo ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 99 na kugharimu jumla ya kiasi cha Shilingi 100,000,000. Nyumba hiyo itaongeza ari kwa walimu watakao kuwa wanafundisha katika sekondari hiyo
Naye Katibu Tawala Wilaya ya Geita Bi Lucy Beda alisema ukamilishwaji wa mradi huo utaongeza ari kwa walimu kufanya kazi vizuri kwani serikali inatenga fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali inayotekelezwa ndani ya halmashauri ya Wilaya ya Geita na kutoa wito wa kuendelea kuilinda na kuitunza.
Ziara hiyo iliendelea kwa kukagua miradi mingine ikiwepo ujenzi wa Zahanati ya Nkome ambao ujenzi huo unatarajiwa kukamilishwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi 2024 na kumtaka Mkandarasi kuongeza kasi kwa kuwa wananachi wanauhitaji wa kituo cha afya. “Mhe Rais amewezesha mazingira bora ya uwekezaji hivyo kasi iongezeke kazi zifanyike usiku na mchana” alisema Mwenyekiti huyo.
Kamati ya Siasa ikikagua ujenzi wa Zahanati ya Nkome unatekelezwa kwa fedha za CSR kiasi cha Milioni 728 ambapo gharama hizo ni za ukamilishaji wa jengo la OPD, Labaratory Block, Maternity Block na Threatre Block
Mradi huo wa Zahanati ya Nkome unatekelezwa kwa fedha za CSR kiasi cha Milioni 728 ambapo gharama hizo ni za ukamilishaji wa jengo la OPD, Labaratory Block, Maternity Block na Threatre Block.
Mradi mwingine ambao kamati ya siasa iliutembelea ni mradi wa maji na jengo la utawala shule ya sekondari Kasoji kata ya Katoma ambao unaendelea na hatua za ujenzi huku Diwani wa kata hiyo ya Katoma Mhe Josephat Omanja akiishukuru serikali kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kutoa fedha nyingi kutekeleza miradi ya maendeleo katika kata hiyo ya Katoma.
Akizungumza na wananchi kwenye ukaguzi wa ujenzi wa mradi huo Mkuu wa Wilaya ya Geita ndugu Cornel Magembe alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni 2024 ambapo kata zitakazo nufaika na maji safi na salama ni Nkome, Katoma, Nyamboge,Nzera na Lwezera na kuwataka wananchi kutunza miundombinu ya mradi huo mkubwa ambao chanzo cha fedha za mradi ni kutoka mfuko wa maji wa taifa (NWF). Ukamilishwaji wa mradi huo utapelekea kuwahudumia wananchi wasiopungua 124,629 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Ujenzi wa mradi wa maji ulipo kata ya Katoma unaotarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni 2024 ambapo jumla ya kata 5 zitanufaika na maji safi na salama ambazo ni Kata ya Nkome, Katoma, Nyamboge,Nzera na Lwezera
Katika mradi wa ujenzi wa jengo la utawala katika shule ya sekondari Kasoji kwenye kata hiyo ya katoma unaogharimu kiasi cha shilingi 92,410,613 kutoka mfuko wa TASAF huku kiasi cha shilingi 5,350,000 zikiwa nguvu za wananchi, kamati hiyo ilipongeza usimamizi mzuri unaofanywa na Halmashauri na kusema dosari ambazo zimeonekana ziweze kufanyiwa kazi kwa uharaka kukamilisha ujenzi huo.
Miradi mingine iliyotembelewa na kamati ya Siasa ya Wilaya ni pamoja na Shule ya Msingi Bwawani inayojengwa kwa fedha za CSR kiasi cha shilingi 300,000,000 ambao umefikia asilimia 75 ya utekelezaji,Shule ya sekondari Kagege uliogharimu kiasi cha shilingi 584,000,000 na shule ya msingi afya ambayo ni nguvu za wananchi zote zikiwa kata ya Ludete, Mradi wa maji mji mdogo wa Katoro ambapo unatekelezwa kwa Force Account na Mamlaka ya majiSafi na usafi wa Mazingira Geita kwa gharama za shilingi 6,117,314,331 huku kiasi cha shilingi 5,882,314,331 kutoka Serikali kuu zikiwa tayari zimepokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita Komredi Mapande akiwa na wajumbe wa kamati ya siasa walipotembelea ujenzi wa mradi wa shule ya msingi Bwawani ambapo alielekeza mafundi kufanya kazi kwa ufanisi na kuitaka Halmashauri kusimamia na kufuatilia mkandarasi anayetekeleza mradi huo, Aidha alitoa rai kwa Wabunge kuangalia upya sheria ya CSR ili mapungufu yaliyopo yarekebishwe kuepuka kucheleweshwa kukamilishwa kwa miradi
Wakihitimisha ziara hiyo ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa ndani ya Halmashauri ya Geita, Kamati hiyo iliwataka watendaji wa Halmashauri kuendelea kusimamia vema na kufuatilia kila hatua ya utekelezaji wa miradi inayoendelea ili kukamilishwa kulingana na thamani ya fedha zinazotolewa na Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Geita ndugu Cornel Magembe akimtwisha ndoo ya maji Mwananchi wakati Kamati ya Siasa ya Wilaya ilipofanya ziara kata ya Katoro. Wananchi hao waliishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwatatulia changamoto ya maji ambayo ilidumu kwa muda mrefu
Mkuu wa Wilaya ndugu Cornel Magembe aliishukuru kamati hiyo ya Siasa kwa ziara waliyoifanya ndani ya Halmashauiri ya Wilaya ya Geita na kuahidi yale yote ambayo kamati hiyo imeelekeza kwa ajili ya maboresho katika miradi yote yatafanyiwa kazi na wataalam kutoka Halmashauri pamoja na kuendelea kuitunza miradi hiyo. Pamoja na hayo aliishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha nyingi Wilayani Geita kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa