Na:Hendrick Msangi
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Geita limefanya mkutano wake Novemba 15 na 16 ,2023 wa Robo ya Kwanza ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 (Julai – Septemba 2023) katika ukumbi wa mikutano wa Halmashuri hiyo iliyopo Kata ya Nzera wilayani Geita na kupitisha taarifa ya utendaji kazi kwa robo hiyo kwa kata zote 37 za Halmashauri hiyo.
Kikao hicho kilichofanyika kwa siku mbili kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali pamoja na wakuu wa idara mbalimbali katika Halmashauri hiyo chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Charles Kazungu ambaye pia ni diwani wa kata ya Butobela.
Aidha, katika kikao hicho ambacho siku ya kwanza kilianza na uwasilishwaji wa taarifa za utekelazaji wa shughuli za maendeleo ngazi ya kata kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2023 na siku ya pili kwa Wenyeviti wa Kamati za kudumu za Halmashauri kuwasilisha taarifa za kamati zao na wajumbe wa Baraza la Madiwani kuzipokea na kuzipitisha kwa pamoja.
Awali akifungua Kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo aliwataka waheshimiwa madiwani kusikiliza na kuuliza maswali au kutoa maoni na ushauri katika taarifa hizo ambazo ziliwasilishwa.
Akizungumza katika baraza hilo Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Geita Cornel Maghembe aliwapongeza madiwani hao pamoja na watumishi wa Halmashauri hiyo kwa utendaji mzuri katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuendelea kusimamia vizuri shughuli zote za Halmashauri . Pamoja na hayo aliwaagiza Madiwani hao kukaa kwa pamoja na kuona namna ya kutatua migogoro inayojitokeza kwenye vijiji na kata zao ili wananchi waendelee kuwa na Imani na serikali yao inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akiendelea kutoa hotuba yake, aliziagiza Taasisi za TARURA na RUWASA ambazo zinagusa wananchi moja kwa moja kuhakikisha wanatatua changamoto kwa wananchi
Nayo kamati ya Siasa ya Wilaya ilisema imeridhika na shughulizi za utendaji katika Halmashauri hiyo na kuitaka Halmashauri kuendelea kuwasaidia Madiwani kuzitatua changamoto zilizodumu kwa muda mrefu kwa wananchi ikiwepo migogoro katika kata zao.
Pia ilitoa maelekezo kwa Wakala wa barabara za vijijini na mijini (TARURA) kuwa na mpango wa muda mrefu hasa kwa barabara zenye changamoto. “Wekeni mipango ya muda mrefu kwa barabara zinazohitaji dharura badala ya kusubiri mpango wa bajeti 2023/24” alisema Cde. Barnabas Mapande ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita.
Kamati hiyo pia iliagiza kero ya kutokuwepo kwa walimu wa jinsi ya kike kwenye baadhi ya shule itatuliwe mapema ikiwa ni pamoja na kuwaajiri walimu wa muda mfupi wakati serikali ikiwa kwenye mpango wa kuleta walimu wa kudumu katika shule hizo ili kupunguza utoro kwani kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na afisa elimu msingi Mwalimu Ibrahimu Bunangoi wa halmashauri hiyo,ilisema Halmashauri inahitaji walimu 6416 na kwa sasa idadi ya walimu shule za msingi ni walimu 3102.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halamashauri ya Wilaya ya Geita Bi. Sara Yohana amelishukuru baraza kwa pongezi na kuwaahidi waheshimiwa madiwani kuwa Halmashauri itaendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa kushirikiana na Madiwani hao ikiwa ni pamoja na kufuata maelekezo ya kiutendaji yaliyotolewa na baraza hilo
Akifunga kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe. Charles Kazungu amewashukuru Waheshimiwa Madiwani na Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kushiriki katika baraza hilo huku akiwataka kuendelea kutekeleza yote ambayo yamejadiliwa ili kutimiza azma ya chama na serikali kwa wananchi.” Uadilifu ndio msingi mkubwa wa utumishi wa umma “alisema Mhe. Kazungu akifunga kikao hicho cha baraza la madiwani robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2023/24 la Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa