Dodoma-Tanzania
Uongozi wa Mkoa wa Geita umekutana na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, ,Wabunge wa Geita pamoja na wawakilishi wa GGML kwa lengo la kupata muafaka kuhusu changamoto za utekelezaji wa miradi ya CSR na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wananchi wa Geita wananufaika ipasavyo na rasilimali za madini.
Akiongoza Kikao hicho Aprili 14, 2025 Jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde (MB),katika kujadili utekelezaji wa miradi ya Mpango wa Uwajibikaji wa Mmiliki wa Leseni kwa Jamii (CSR) inayotekelezwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) katika Mkoa wa Geita Waziri Mavunde amesisitiza kuwa wananchi wa Geita wanatamani kuona matokeo ya moja kwa moja ya uwepo wa mgodi huo kwa kupitia miradi ya maendeleo.
"Nimeitisha kikao hiki kwa lengo la kutafuta njia bora ya kutekeleza miradi ya CSR, kutatua changamoto zilizopo, na kuhakikisha wananchi wa Geita wananufaika na rasilimali zinazochimbwa katika maeneo yao.”Amesema Mhe Mavunde.
Aidha Mhe Mavunde amesema upo umuhimu wa kukamilisha utekelezaji wa miradi ya nyuma ya kuanzia mwaka 2018-2021 ili kuwezesha uanzishwaji wa miradi mipya yenye tija kwa jamii.
Pamoja na hayo Mhe Mavunde ametoa agizo la siku tatu kwa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kukutana na Wakurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita, kwa lengo la kuandaa na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya nyuma
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Anglo-Gold Ashanti, Simon Shayo, amesema kwamba Kampuni ya GGM ipo tayari kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Geita kuhakikisha wananchi wa Geita wananufaika na miradi ya CSR ambayo kwa sasa kwa ujumla wake imetengewa kiasi cha Tsh 21bn kwa ajili ya utekelezaji wake na hivyo kuleta matokea chanya kwenye. maendeleo ya mkoa wa Geita
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella, ameisisitiza GGML kuhakikisha miradi iliyosainiwa inatekelezwa kwa wakati na kwa mujibu wa makubaliano, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya Mgodi na Uongozi wa Mkoa kwa manufaa ya wana Geita.
Wakichangia kwenye kikao hicho wabunge wa Mkoa wa Geita Mh. Constantine Kanyasu,Mh. Joseph Kasheku Msukuma na Mh. Tumaini Magesa wameitaka Kampuni ya GGML kuhakikisha inakamilisha miradi ya CSR kwa wakati na kwa ubora wa juu utakaoendana na gharama zilizotumika ili wananchi wa Geita wayaone matunda ya uwepo wa Mgodi huo.
Kwa sasa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) huchangia kiasi cha Shilingi bilioni 9.2 kila mwaka kama sehemu ya CSR Mkoani Geita ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Geita hupokea kiasi cha shilingi 4.3 na Manispaa ya Geita kiasi cha shilingi Bilioni 4.9.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa