Wananchi wa kata ya Lubanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita wametakiwa kuharakisha ujenzi wa choo na nyumba ya mganga ili Zahanati yao ianze kufanya kazi ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.
Hayo yamebainishwa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupitia kwa Afisa Mipango wake Bi.Kashinje Bukombe alipoambatana na kamati ya Siasa ya Wilaya kutembelea mradi huo Septemba 16,2021.
Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Mh.Alexander Buteyeye amesema kuwa watatekeleza agizo hilo la Serikali kwa kukaa vikao na kuweka mikakati ya kukamilisha ujenzi huo ili huduma zianze kutolewa kwa wananchi.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya Beatrice Munisi alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) wa kuhakikisha kila kata ina kituo cha Afya ambapo mpaka sasa mradi huo umegharimu jumla kiasi cha shilingi 87,220,354.
Aidha Halmashauri ya Wilaya ya Geita imepanga kukamilisha kituo hiki kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ukamilishaji wa jengo la OPD,Nyumba za Watumishi ,ujenzi wa choo na kichomea taka utakamilishwa kufikia desemba 2021 kupitia fedha zilizotolewa na TAMISEMI kiasi cha shilingi 50,000,000 huku majengo mengine ya kituo yakikamilishwa baadae kadri fedha zitakavyopatikana.
Naye mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Barnabas Mapande ameiomba Halmashauri ya Wilaya hiyo kuandaa mpango unaoonyesha ni kwa namna gani Serikali itakamilisha miundombinu iliyobaki.
Aidha kukamilika kwa Mradi huo wa Zahanati kunategemea kuwanufaisha wananchi wa Lubanga na vijiji jirani vyenye zaidi ya wakazi 19,085 kupata huduma za Chanjo,Afya ya uzazi ,Wagonjwa wa nje,Uzazi wa mpango na Upimaji wa Virusi vya UKIMWI kwa karibu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa