Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Geita imeziomba taasisi za umma kuendeleza dawati la TEHAMA hata baada ya wiki ya TEHAMA kuisha kwa lengo la kuendelea kuielimisha jamii, kwa kuwa Ulimwengu wa sasa uko katika mageuzi makubwa ya TEHAMA.
Akizungumza katika kilele cha wiki ya TEHAMA ki Wilaya kilichofanyika leo ijumaa Oktoba mosi katika ukumbi wa GEDECO kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Geita Bw.Thomas Novatus Festus amesema kuwa licha ya wiki ya TEHAMA kufikia kilele chake hii leo ni vyema madawati ya TEHAMA yakaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu maendeleo ya Sekta hiyo.
Bw.Thomas amesema kuwa zaidi ya watu 475 kutoka makundi ya Jumuiya ya wafanyabiashara, vikundi vya wakulima, vikundi vya mikopo, wasanii, wamachinga, vikundi vya Ushirika, wanafunzi na walimu wamepata Semina kuhusu TEHAMA.
Ameendelea kusema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ilipanga kuwa na wiki ya TEHAMA kuendana na kauli mbiu ya mbio za Mwenge maalumu wa Uhuru 2021 inayosema ‘’TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu itumie kwa usahihi na uwajibikaji’’
Aidha amesema kuwa katika kuadhimisha wiki ya TEHAMA wamefanikiwa kutoa elimu ya TEHAMA inayoendana na kauli mbiu ya mbio za Mwenge maalumu wa Uhuru kupitia semina, magari ya matangazo, tovuti ya Halmashauri, na redio yetu pendwa ya Rubondo fm.
Sanjari na hayo Bw.Thomas amewaomba wananchi wote kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika mbio za Mwenge maalumu wa Uhuru mwaka 2021 kwa kuupokea ,kuukimbiza na mkesha wake utakuwa katika Mji mdogo wa Katoro siku ya Octoba 12, 2021
Wiki ya TEHAMA ki Wilaya ilianza rasmi jumatatu ya Septemba 27 ambapo kwa muda wote huo timu ya uhamasishaji na matumizi sahihi ya TEHAMA ilikuwa ikipita kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu kabla ya kufikia kilele chake hii leo Oktoba Mosi 2021.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa