Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba ameongoza mamia ya Wananchi Mkoani Geita Katika Maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika ukumbi wa GEDEKO Mkoani Geita Disemba 9, 2024.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Geita Ndg Herman Matemu alisema Uhuru wa Tanzania haukupatikana kirahisi bali ulikuwa ni mchakato wa muda mrefu na kuwataka wananchi kuendelea kuwa enzi waasisi wa Uhuru. “Tupo huru na maendeleo yanafanyika hivyo tuendelee kuwa na jukumu la ku enzi viongozi wetu waliomwaga damu kuipambania nchi yetu” Amesema Mtemu
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba akizungumza mbele ya wageni waalikwa na wananchi katika hafla ya maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru.
Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Martine Shigela, Mhe Komba katika hotuba yake amezungumza na wazee ambao walikuwepo kabla ya Uhuru ili kuwaelezea wananchi waliohudhuria katika kongamano hilo hali ilivyokuwa kabla ya uhuru na hali ilivyo kwa sasa katika Serikali.
Wakizungumza wakati wa Maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru yaliyofanyika katika Ukumbi wa GEDEKO Mkoani Geita wazee hao wamesema miaka ya nyuma kabla ya Uhuru Geita wakati huo ikiwa ni Wilaya haikuwa na huduma za kijamii kama shule na hospitali na badala yake walilazimika kwenda Mwanza ila kwa sasa Serikali Inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya kazi njema zilizo asisiwa na waasisi na katika kusherehekea miaka 63 ya Uhuru kila kata ina shule, zahanati na vituo vya afya ni vingi.
Wazee mbalimbali wa umri wa zaidi ya miaka 63 wakizungumza mbele ya kongamano, tofauti ya kimaendeleo iliyopo mara baada ya Uhuru wa Tanzania bara, na sasa
Aidha wazee hao wamewataka vijana kuacha kuilalamikia serikali kwamba haileti maendeleo kwenye jamii zao badala yake waiunge mkono izidi kuleta maendeleo kwani mpaka sasa Tanzania imepiga hatua kubwa ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali
Pamoja na hayo Mhe Komba ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuwa wazalendo, kujituma, kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwani miaka 63 ya uhuru imekuwa na ushindi katika sekta mbalimbali za maendeleo.” Mimi na wewe tujiulize tunafanya nini, tuendelee kuwa na tafakari ya kina tumetoka wapi na tunaenda wapi” amesema Kaimu Mkuu wa Mkoa Mhe Komba.
Katika Maadhimisho hayo mada mbalimbali ziliwasilishwa katika kuulezea umma namna ambavyo Taifa lilipitia michakato mbalimbali katika Kupata Uhuru.
Kwa upande wake Mwalimu Isdory Vitus Kalimuwabu kutoka shule ya Sekondari Mwatulole alizungumzia mada ya Historia ya harakati za kupata Uhuru wa TanzaniaBara na Mchango wa Viongozi wa Taifa katika maendeleo ya kiuchumi Tanzania na kuelezea hatua mbalimbali zilizopitiwa hadi kupata uhuru.
Mada nyingine iliyozungumziwa katika Kongamano hilo ni Tanzania na harakati za Mapinduzi ya Kiuchumi katika Sekta za elimu, afya, Maendeleo ya jamii, Kilimo, Miundombinu,Nishati, biashara, mawasiliano na ujenzi iliyo wasilishwa na Ndg ALLY Abuu Kutoka chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT).
Pamoja na mada hizo, Ndg Kadole Ngumungu ambaye ni Afisa Utumishi na Rasilimali watu Halmashauri ya Mji Geita aliwasilisha mada isemayo Hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ukuaji wa siasa na maendeleo ya Taifa huku Afisa Maendeleo ya Vijana Mwandamizi Ndg Zengo Polle akiwasilisha mada ya Uhuru na maadili ya Taifa katika kuchochea fikra za kizalendo na masuala ya uongozi kwa vijana.
Maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru mwaka huu yamebebwa na Kauli mbiu isemayo, “Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara: “UONGOZI MADHUBUTI NA USHIRIKISHWAJI WA WANANCHI NI MSINGI WA MAENDELEO YETU.”
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa