WAZAZI nchini wameaswa kuzingatia lishe bora ili kuwezesha upatikanaji wa maziwa ya kutosha na yenye ubora pindi wanapowanyonyesha watoto wachanga ili kusudi waweze kuwa na afya bora.
Hayo yamesemwa Agosti 07, 2024 na Afisa Lishe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bi Umi Zuberi Kileo katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya unyonyeshaji Maziwa ya Mama pamoja na kutoa elimu ya uzazi salama yaliyofanyika katika Zahanati ya Kata ya Lwezera ambapo amewasisitiza akina mama kuhakikisha wanapata lishe bora muda wote ambao wanakua katika kipindi cha unyonyeshaji wa mtoto.
Bi Umi Kileo ambeye ni Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita akielezea umuhimu wa lishe bora kwa mama anaye nyonyesha ambapo amewataka wazazi kuzingatia lishe iliyo bora ili kusudi waweze kutoa maziwa yenye ubora na ambayo hayataweza kumletea madhara ya kiafya mtoto mchanga.
"Mzazi anapaswa azingatie kua anapata lishe iliyo bora ili kusudi aweze kutoa maziwa yenye ubora na ambayo hayataweza kumletea madhara yeyote ya kiafya mtoto mchanga.”Amesema Bi Umi.
Aidha Afisa Lishe huyo amewaeleza wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo kuwa maziwa ya mama yanasaidia kumpa kinga madhubuti mtoto pindi anapokua amezaliwa na mama anapaswa kumyonyesha kwa angalau miezi sita pasipo kumpa kitu kingine.
Wananchi kutoka maeneo mbalimbali wakifuatilia masomo ya lishe bora kwa wazazi wakati wa maadhimisho ya kilele cha wiki ya unyonyeshaji Maziwa ya Mama duniani ambapo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita yamefanyika kata ya Lwezera.
Pamoja na hayo Bi Umi amewasihi akina mama kuendelea kuwanyonyesha watoto kwani kwa kufanya hivyo wataendelea kuboresha afya zao.
Kwa upande wake, Bi Theresia Simon ambae ni Afisa Muuguzi, ameishukuru Halmashauri ya Wilaya kwa kupitia Wizara ya Afya, kuandaa programu hiyo pamoja na kuitaka iwe endelevu kwa kuwa akina mama wanaojifungua ni wengi.
"Huduma hii ikiwa endelevu itaendelea kuleta muitikio kwa akina mama kwa kuwa kila mwezi wamama wanajifungua.” Amesema Bi Theresia huku akishukuru kwa somo zuri lililotolewa juu ya lishe bora.
Maafisa Lishe wakiwaonyesha wananchi waliohudhuria maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji kata la Lwezera namna ya kuandaa uji bora wa lishe. Wazazi wameshukuru kwa mafunzo hayo ya uandaaji wa lishe bora na umuhimu wa mama kunyonyesha mtoto na kuomba somo hilo liwe endelevu kuwasaidia akina mama wanaojifungua kila mwezi
Wakati huo huo Bi Janet Jackson kwa niaba ya akina mama waliojitokeza kwenye program hiyo ameiomba serikali iweze kuwaelimisha zaidi wananchi haswa wanaoishi vijijini ili kuwa na jamii yenye ustawi na afya bora.
"Tunashukuru kwa elimu hii tulioletewa na wahudumu wetu wa afya. Wito ni kuiomba serikali iweze kutoa huduma hii sehemu tofauti tofauti haswa huku sehemu za vijijini ili sote tuwe na afya njema na hili kwa kiasi kikubwa litasaidia kuwa na jamii yenye afya njema. " Amesema Bi Janet.
Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama huadhimishwa duniani kote kuazia tareh 1-7 Agosti kila mwaka kwa lengo la kusisitiza umuhimu wa kulinda, kuimarisha na kuendeleza unyonyeshaji wa maziwa ya mama, ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu ilikua ni, "TATUA CHANGAMOTO: SAIDIA UNYONYESHAJI WATOTO KWA WOTE."
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa