Kufuatia maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma barani Afrika, Watumishi wa Umma kutoka sekta mbali mbali Mkoani Geita wamehimizwa kuwa wanajifanyia tathmini ili waweze kukidhi sifa za kupanda madaraja.
Akizungumza na Wakuu wa Idara kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita mapema wiki hii katika awamu ya pili ya utoaji wa mafunzo ya utumiaji wa mfumo wa kupima Uwajibikaji na Utendaji wa Watumishi (ESS), Mratibu kutoka Ofisi ya Raisi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ndg. Elibariki Funga, amewasisitiza Wakuu hao wa Idara kuwafanyia tathmini watumishi walio chini yao kwa kuwa ni muhimu ili kuweza kuwaweka kwenye nafasi ya kupanda madaraja pindi muda wa kupanda madaraja utakapowadia.
Aidha, Ndg. Funga pia ameongeza kwa kusema kuwa, lengo kuu la kufanya tathmini miongoni mwa watumishi ni pamoja na kuhakikisha Watumishi wanatekeleza wajibu wao na hivyo wanapaswa kulichukulia jambo hilo kwa uzito mkubwa.
“Kila mtumishi anatakiwa awe na majukumu yake mwenyewe. Hivyo lazima uwepo mpango madhubuti, ndani ya muda husika wa kufanya tahmini kwa Watumishi wa Umma. Tunapaswa kutambua kuwa tunajenga cha kwetu.”
Kwa upande mwingine, Ndg. Raphael Kimaro (Mratibu kutoka Ofisi ya Raisi Menejienti ya Utuishi wa Umma na Utawala Bora) amesema kuwa, nia ya mafunzo hayo ni kuhakikisha yanaleta Utumishi nwenye tija pamoja na kujengeana uwezo ndani ya taasisi husika.
Kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mkuu wa idara ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (M) Ndg. Herman Matemu amewataka Watumishi mkoani humo kujaza majukumu yenye uhalisia lakini pia kuwataka kutoa mrejesho kwa watumishi wanaowasimamia kwa wakati.
Siku ya Utumishi wa Umma husherehekewa Juni 23 kila mwaka na nchi wanachama wa Umoja Wa Afrika kwa kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya nchi zao ambapo kwa mwaka huu iliongozwa na kauli mbiu isemayo: “Himiza matumizi ya mifumo ya kidijiti ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji.”
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa