Katika kuhakikisha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita inapambana na changamoto ya Lishe Duni pamoja na udumavu kwa Watoto chini ya umri wa miaka mitano, rai imetolewa kwa Halmashauri kupitia kwa Idara ya Afya kuhakikisha inashirikiana na Watendaji wa Kata na Vijiji ili Afua za Lishe ziweze kutekelezwa kwa ukamilifu.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba Julai 11, 2025 eneo la Ukumbi wa EPZ-Bombambili, Manispaa ya Geita, katika kikao kazi cha kujadili tathmini ya jumla ya Hali ya Mapato, Miradi, Afua za Lishe, pamoja na changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi na Kamati ya Usalama ya Wilaya, kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akizungumza mbele ya Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Halmashauri ya Wilaya na wa kutoka Manispaa ya Geita, Mhe. Komba amesema kuwa Halmashauri zina wajibu wa kuhakikisha zinawasimamia Watendaji wa Kata na Vijiji pamoja na kutoa fedha mapema kwenye mipango ya Lishe inayohitaji utekelezaj wa haraka.
Mhe. Komba pia ametoa pongezi kwa Maafisa Lishe wa Wilaya kwa kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Mkakati wa Lishe wa Taifa (NMNAP II) wa kupambana na tatizo la Lishe Duni sambamba na la Utapiamlo na Aina zake (Triple Burden of Malnutrition), huku lengo likiwa ni kuhakikisha jamii inakuwa na elimu ya kutosha juu ya ulaji wa vyakula vyenye virutubisho ili kuondokana na matatizo yanayosababishwa na Lishe Duni.
Naye Afisa Lishe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bi. Umi Kileo amesema kuwa miongoni mwa mafanikio yaliyoweza kufikiwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ni pamoja na kutoa matibabu kwa Watoto 86 ambao waliibuliwa katika jamii kwenye zahanati na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya Nzera, Hospitali ya Katoro, na Kituo cha Afya Kasota ambapo walitibiwa kwa kutumia fomula ya vyakula dawa vilivyotengenezwa wodini.
Aidha, Halmashauri pia inaendelea na programu ya Jiko-Darasa kwenye zahanati na vituo vya afya ili kuwajengea uwezo wazazi pamoja na walezi jinsi ya kuboresha vyakula vya Watoto, hali itakayosaidia kupunguza athari za utapiamlo, na pia kusaida mwendelezo wa elimu kila hudhurio kwa wazazi na walezi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa