Na: Hendrick Msangi
Katika Kikao elekezi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kati ya Watendaji wa Kata na Vijiji pamoja na Timu ya Menejementi ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita , watendaji wa kata na vijiji wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kuiletea Halmashauri sifa njema na kuinua mapato ya Halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita yenye jumla ya kata 37 na vijiji 145 shughuli kubwa za uzalishaji zikiwa ni kilimo, ufugaji, uvuvi uchimbaji madini na viwanda vidogo huifanya Halmashauri kupata mapato yake yake ya ndani kupitia shughulizi zinazofanyika ndani ya kata zote 37.
Ili kuendelea kusimamia vyanzo vya mapato na kuongeza pato la Halmashauri, watendaji wa kata na vijiji wametakiwa kujituma na kuwatumikia wananchi katika maeneo yao ikiwa na ni pamoja na kuwa na njia nzuri za ukusanyaji wa mapato.
Akizungumza na watendaji hao katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, Afisa Kilimo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Dkt Alphonce Bagambabyaki amewataka watendaji hao kuwahimiza maafisa mifugo walio kwenye kata zao kukusanya mapato ya ada ya ukaguzi baada ya kukagua nyama ili kuendelea kuongeza mapato katika chanzo hicho.
Aidha kwa upande wa ushuru wa mazao ya samaki, watendaji hao walielekezwa kutoza ushuru kuanzia kilo moja ya samaki kwa shilingi 100 na kuwataka kuwajulisha maafisa uvuvi pindi wanapotaka kufanya doria za kwenye maji.”Ni kosa kwa watendaji kufanya doria kwenye maji bila kuwepo kwa Afisa Uvuvi” alisema Dkt Alphonce.
Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita walipozungumza na Watendaji wa Kata na Vijiji kuwapa maelekezo katika kuileta Halmashauri sifa njema katika utendaji kazi wao.
Pamoja na hayo watendaji hao wametakiwa kutokukata stakabadhi ya mazao ya kilimo bila kushuhudia gari lililobeba mazao ili kuepuka kukata ushuru pasipo kujiridhisha na kuwataka kuwepo kwa watu kwenye vizuizi (Barrier ) muda wote kwani asilimia Zaidi ya 70 ya mazao yanasafirishwa usiku na kutakiwa pia kukatiwa ushuru kwa mazao yote yanayosafirishwa na bodaboda au maguta kwa kuwa imebainika wengi hutumiwa na wafanyabiashara kusafirisha mazao hayo kutoka eneo moja kwenda lingine na kukwepa kulipa ushuru.
Kwa upande mwingine watendaji hao wametakiwa kuhakikisha wanafanya vikao vya kisheria, kusoma mapato na matumizi katika maeneo yao, kusimamia mahudhurio ya watumishi walio chini yao na kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo katika kata zao kwa kuzisimamia kamati za miradi kwani wao ni wadau wakubwa katika miradi inayoendelea kwenye kata zao hivyo kutakiwa kusimamia maboma yanayoanzishwa na wananchi yawe na ubora sawa na majengo ya serikali.
Watendaji wa Kata na Vijiji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakipokea maelekezo kutoka kwa timu ya menejimenti ambapo wametakiwa kuwa waadilifu katika utendaji wao ili kuendelea kuinua mapato ya Halmashauri ikiwa ni mapoja na kusimamia miradi yote ya maendeleo katika maeneo yao.
Akiwapa maelekezo hayo Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Dominic Shilingo amewataka watendaji hao kuwa na ushirikiano pale fedha za miradi zinapoingia kwenye kata zao, na kuhakikisha vifaa vya ujenzi vinakaguliwa ili kuwa na ubora unaostahili pamoja na kuzingatia thamani ya soko kuepuka kuweka maslahi mbele kwa fedha za serikali na kuwataka kuwashirikisha wananchi kushiriki katika miradi ya maendeleo katika maeneo yao. Aidha Mhandisi Shilingo aliwataka watendaji hao kufuatilia vibali vya ujenzi unaoendelea kwenye maeneo yao kwani ni chanzo cha mapato ya halmashauri.
Swala la lishe kwa wanafunzi nalo halikuachwa nyuma ambapo watendaji hao walitakiwa kulipa kipaumbele kwani ni agizo la serikali wanafunzi wapate lishe wawapo shuleni,
Akizungumza katika kikao elekezi hicho kwa niaba ya Mkuu wa Divisheni ya Elimu awali na msingi Mwalimu Neema Mwaluko alisema ofisi ya Mkurugenzi inaendelea kuwashukuru watendaji hao kwa kazi nzuri ya kuhamasisha swala la lishe shuleni kwani ongezeko la shule zinazotoa lishe kwenye halmashauri zimeongezeka kutoka shule 84 hadi shule 178 kati ya shule 235 za serikali na kuwataka kuendelea kuelimisha wazazi kuchangia chakula kwani ni agizo la serikali jamii ichangie ili watoto wapate chakula shuleni.
Watendaji wa kata na Vijiji kwa pamoja wameazimia kutekeleza na kuyasimamia yote waliyoelekezwa na uongozi wa Halmashauri ili kuendelea kuipa sifa njema Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Aidha Mwl Neema aliwataka watendaji hao kuendelea kusimamia swala la utoro shuleni kwa kuweka mikakati ya kupunguza utoro kwani Halmashauri inakabiliwa na utoro mkubwa wa wanafunzi sawa na asilimia 11 kulinganisha na Halmashauri nyingine. Pamoja na hilo watendaji hao walitakiwa kusimamia swala la ulinzi na usalama kwenye shule kwani zipo baadhi ya shule kuvamiwa na wananchi. “Inasikitisha mahindi na vifaa vinaibiwa, wapo pia walimu ambao wanavamiwa na kuibiwa mali zao, mkaimarishe ulinzi kwa kuweka mikakati na kuepusha tabia hizo za uvamizi” alisema Mwl Neema.
Akifunga kikao hicho kwa niaba ya Mkuregenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bi Sarah Yohana ambaye ni Mkuu wa Idara ya Mipango amewataka watendaji hao kutekeleza yote waliyoelekezwa na kuazimiwa ili kuendelea kuipa halmashauri sifa njema katika kuinua mapato.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa