Na Hendrick Msangi
WATENDAJI wa Vijiji wa Halmashauri ya wilaya ya Geita , Desemba 18, 2023 wamepatiwa elimu juu ya utunzaji wa Mazingira na usafi katika maeneo yao ili wakawe mabalozi wazuri kwa wananchi wanaowasimamia
Hayo yameelezwa na Afisa Afya Halmashauri ya Wilaya ya Geita Kimwago Singo wakati wa kikao na watendaji hao ambapo watendaji hao walielekezwa kuhamasisha jamii kuwa na vyoo na kuvitumia ili kuyatunza mazingira.
Afisa Afya ndugu Kimwago Singo akitoa elimu kwa watendaji wa vijiji juu ya matumizi ya vyoo bora na umuhimu wa kuyatunza mazingira kwa kuzingatia matumizi sahihi ya vyoo.
Aidha Afisa Afya huyo, alisema wananchi wanapaswa kushirikishwa katika kutengeneza miundombinu ya vyoo na matumizi bora ya huduma za usafi wa mazingira kwa kuendelea kuwajengea uelewa.
“Tunapofanya kazi pamoja kama jamii na kuchukua hatua za kuleta mabadiliko katika suala la afya ya binadamu na mazingira, kupitia elimu tunayopeana , ubunifu pamoja na ushirikiano na viongozi ngazi ya jamii , tunaweza kufikia lengo la kila kaya kuwa na vyoo bora na kuchangia katika maendeleo endelevu katika halmashauri yetu,” alisema Singo.
Pamoja na hayo Afisa Afya huyo alisema kupitia program ya huduma ya maji safi vijijini (SRWSS) halmashauri ya wilaya ya Geita hupokea fedha kutokana na ufaulu wa uhakiki wa uwepo wa vyoo bora ngazi ya jamii unaofanyika kwa ngazi ya jamii kwa ajili ya utekelezaji wa huduma endelevu za maji safi na usafi wa mazingira vijijini chini ya ufadhili wa Benki ya dunia ambapo alisema kaya zote, taasisi na nyumba za ibada zinatarajiwa kuwa na vyoo 100% ifikapo Disemba 30, 2023
Mwisho Afisa afya huyo aliwataka watendaji hao kulifanya zoezi la utoaji elimu kwa jamii juu ya matumizi ya vyoo bora kuwa endelevu ili jamii izidi kuona umuhimu wa kuyatunza mazingira kwa kuzingatia matumizi sahihi ya vyoo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa