Na Hendrick Msangi
Katika kuhakikisha Halmashauri ya Wilaya ya Geita inafikia malengo katika utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe, Watendaji wa Vijiji vya Halmashauri hiyo wameendelea kuhamasishwa kuwasaidia wananchi katika maeneo yao ili watekeleze afua hizo kwakuwa mabalozi wazuri kwa jamii inayowazunguka kutambua umuhimu wa lishe bora.
Hayo yameelezwa Desemba 18, 2023 wakati wa kikao cha Maafisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Watendaji wa Vijiji kujadili Mkataba wa Lishe katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo kata ya Nzera Wilayani Geita.
Awali akifungua semina hiyo elekezi Msimamizi Mkuu wa shughuli za afya, Lishe na Ustawii katika Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita Dkt Modest Buchard alisema jamii inapaswa kuwa na uelewa mpana kuhusu maswala ya Lishe ili kupunguza na kumaliza athari za utapiamlo katika jamii ikiwa ni pamoja na kuwataka watendaji hao kuwa mabalozi kwa kuhakikisha wanatoa elimu wanayoipata kwa kufuatilia huduma za afya na lishe kwa mama na mtoto kwa kuihamasisha jamii kushiriki vema bila kuacha ushiriki wa baba katika maswala yote ya lishe kwa kuzingatia kunakuwepo na ulaji mzuri na wenye kuzingatia vyakula venye faida katika mwili
Naye Afisa Lishe Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Umi Zuberi Kileo alisema kulingana na Mkataba wa lishe ambao kwa awamu ya tatu ulisainiwa Septemba 30,2022 baina ya Mhe Rais na wakuu wa Mikoa ulielekeza wajibu kwa watendaji wote kwa kuhakikisha ajenda ya lishe inakuwa ya kudumu katika vikao vya Halmashauri ya kijiji, kuchochea na kuibua fursa za lishe ikiwa ni pamoja na kutatua matatizo ya lishe kwenye jamii zao kwa kuhakikisha shughuli za lishe zinatolewa taarifa pamoja na kuwatambua wadau wote kwenye ngazi ya kijiji.
Aidha Bi Umi aliendelea kusema , Mkataba huo unatoa wajibu kwa kijiji kukusanya, kutathmini na kujadili taarifa za lishe kutoka kwenye kaya na maeneo mengine ndani ya kijiji pamoja na kuhakikisha mpango kazi wa lishe unajumuisha afua za chakula na lishe,afya, maji safi na usafi wa mazingira na uchangamshi kwa watoto wadogo.
Maafisa Lishe wakimpima urefu mtoto mbele ya watendaji wa vijiji wakati wa semina ya kuwajengea uelewa maswala ya lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita Desemba 18, 2023
Pamoja na kueleza wajibu wa kijiji kutokana na mkataba huo, Bi Umi aliwaeleza watendaji hao kwamba wanapaswa kushirikiana kufanya kazi kwa ufasaha ili kufikia malengo ya mkataba huo kwa kuhakikisha wanaongeza kasi kwa watoa huduma ngazi ya jamii ili kuwafikia walengwa kuongeza hamasa na ushiriki wa jamii ikiwa ni pamoja na kuongeza mwitikio na uwajibikaji wa viongozi katika usimamizi na utaratibu wa huduma za lishe kwa ngazi ya kijiji.
Afisa Lishe huyo aliwataka watendaji hao kuwaalika watoa huduma ngazi ya jamii katika mikutano ya hadhara kila mara wanapokutana na wananchi ili kuweza kuendelea kuijengea jamii uelewa wa maswala ya lishe. Pia aliwashauri watendaji hao kuielimisha jamii kuweka ziada ya chakula wakati wa mavuno na sio kuuza chakula chote ili kiisaidie jamii kwani ukosefu wa lishe bora husababisha utapiamlo ambao watu wengi katika jamii hudhani kuwa ni ushirikina.
Akiendelea kuwajengea uwezo watendaji hao, Bi Umi Kileo alisema yapo mambo ya kuzingatia katika jamii ili kuzuia utapiamlo ambapo aliwaeleza watendaji hao waendelee kuihamasisha jamii inayowazunguka kuwa na desturi ya kula mlo kamili, kuwaelimisha wajawazito katika maeneo yao umuhimu wa kuanza huduma ya kliniki mapema na kuwa na mahudhurio yanayoshauriwa , ikiwa ni pamoja na ushiriki wa baba katika kuwezesha ujauzito salama na kumpunguzia mama kazi ili kupata muda wa kupumzika kuwezesha uzazi salama “Utapiamlo hauna ushirikina ni kuzingatia Lishe bora ”, alisema Bi Umi akihitimisha mafunzo hayo kwa watendaji wa vijiji.
Watendaji wa Vijiji Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakifuatilia semina juu ya utekelezaji wa Afua za Lishe Katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ambapo walipata kujifunza mambo mengi na kuweka azimio la kuifanya ajenda ya Lishe kuwa ya kudumu kwenye vikao na mikutano ya hadhara
Msimamizi Mkuu wa shughuli za afya, Lishe na Ustawii katika Jamii Dkt Modest Buchard aliwashukuru Watendaji hao kwa kuhudhuria semina hiyo na kuwataka watendaji hao kuwa mabalozi wazuri katika jamii kwa kuifanya ajenda ya lishe kuwa ajenda ya kudumu kila wanapokuwa na vikao au mikutano ya hadhara ili jamii iendelee kuwa na uelewa mpana wa maswala ya lishe pamoja na kuzingatia vyakula venye faida katika mwili.
Mkoa wa Geita ni miongoni mwa mikoa mitano ambayo haikufanya vizuri kwenye swala la lishe. Itakumbukwa katika ziara ya kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (MB), Desemba 16, 2023 alipotembelea Mkoa wa Geita, Mhe Mkuu wa Mkoa wa Geita ndugu Martine Shigela alimueleza Waziri kuwa hatua madhubuti zimeshachukuliwa kwa kuweka mikakati pamoja na kuwa na nyenzo zote zinazohitajika kwenye vituo vya afya ikiwa ni pamoja na kuongeza hamasa kwa jamii kukabiliana na tatizo la Lishe Mkoani Geita.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa