WATENDAJI wa Kata na Vijiji wameaswa kusimamia maswala ya utawala bora katika maeneo yao ya utawala ili kuendelea kudumisha amani na utulivu.
Akizungumza na watendaji wa kata na vijiji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Januari 28, 2025 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita-Nzera, Afisa TAKUKURU Mkoa wa Geita Ndg Maganga Lutunge amewataka watendaji hao kusimamia wajibu na majukumu katika Kusimamia utawala bora ili kudumisha amani katika jamii wanazozimamia na kuziongoza na kuepusha vurugu zinazoweza kurudisha maendeleo nyuma.
Afisa TAKUKURU Mkoa wa Geita Ndg Maganga Lutunge akizungumza na watendaji wa kata na vijiji Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambapo amewataka watendaji hao kusimamia wajibu na majukumu katika Kusimamia utawala bora
“Taasisi ya TAKUKURU imepewa mamlaka ya kudhibiti vitendo vya rushwa vinavyopelekea uvunjifu wa amani ambayo husababishwa na utawala mbovu hivyo tuzingatie utawala bora” Amesema Lutunge.
Vilevile Ndg Lutunge ameongeza kwa kusema vitendo vya rushwa, ubadhilifu, unyanyasaji wa wananachi, huduma duni, kutokujali wananchi, kutokuwajibika, wananchi kutokushirikishwa katika maamuzi yanayowahusu katika kutekeleza malengo ya serikali na kudumisha ustawi wa wananchi yanapaswa kuepukwa kwa kuweka na kuzingatia misingi ya utawala bora.
“Mambo mawili ya kuzingatia ili kuepuka rushwa ni kuzingatia sheria inayosimamia kazi au majukumu yenu pamoja na kuepuka kujipatia manufaa kwa kuvunja sheria kwako au kwa mtu mwingine”
Halikadhalika Watendaji wa Kata na Vijiji wamepewa elimu ya namna ya kusimamia migogoro ya ardhi katika maeneo yao ya kiutawala. Ndg, Alex Robert ni Katibu kutoka Baraza la Ardhi na nyumba Wilaya ya Geita ambapo amewataka watendaji hao kusimamia kikamilifu migogoro ya ardhi kupitia mabaraza ya kata katika maeneo yao ya kiutendaji. “Tuepushe malalamiko kwa kuegemea upande mmoja” Amesema Ndg Alex Robert katika mafunzo hayo.
Ndg, Alex Robert Katibu kutoka Baraza la Ardhi na nyumba Wilaya ya Geita akizungumza na watendaji wa kata na vijiji katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita-Nzera ambapo amewataka watendaji hao kusimamia kikamilifu migogoro ya ardhi
Afisa Ardhi huyo ameongeza kwa kusema mabaraza ya kata yana mamlaka ya kupokea migogoro katika kata husika
“Mabaraza ya Kata yamepewa mamlaka ya usuluhishi tu katika migogoro ya Ardhi baada ya mabadiliko ya sheria ambapo mabaraza ya kata yanatambuliwa na sheria kuu mbili ambayo ni sheria ya mabaraza sura namba 206 toleo la mwaka 2002, sheria ya mahakama za migogoro ya ardhi sura namba 216 toleo la mwaka 2019 inayotoa mamlaka ya Mabaraza kupokea migogoro katika kata zao. ”Amesema Ndg Alex.
Mafunzo hayo yamefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Sheria ambayo kwa Mkoa wa Geita ilizinduliwa na Mhe Martine Shigela Mkuu wa Mkoa wa Geita Januari 26, 2025 huku kauli mbiu ikisema “Tanzania ya 2025, Nafasi ya Taasisi zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo”.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa