Katoro-Geita
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Rajab Magaro leo 1,Machi 2025 ameshiriki katika zoezi la kufanya usafi wa mazingira katika Mamlaka ya mji mdogo wa Katoro.
Akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba katika zoezi hilo la kusafisha mazingira ya Mji huo , Ndg Magaro amewataka wafanyabiasha wa Mji huo kuwa na Utamaduni wa Kufanya usafi katika maeneo yao na ambao watakiuka agizo hilo hatua kali zitachukuliwa juu yao.
" Lazima tuchukue maamuzi magumu ili Mji uwe Msafi kwa kuwapiga faini wale wote ambao watakiuka maagizo ya Serikali kwa kuwapiga faini kwa mujibu wa Sheria" Amesema Magaro.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji ndg Magaro amesema zoezi la usafi ni endelevu na kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuhamasishana kufanya usafi katika maeneo yao ili kuepukana na magonjwa ya milipuko.
" Maeneo mnapofanyia shughuli zenu hakikisheni yanakuwa safi ikiwa ni pamoja na kuepuka kumwaga uchafu kwenye mitaro ya maji ili isizibe ikiwa ni pamoja na kukusanya takataka maeneo yote ya kazi ili zisisambae" Ameongeza Ndg Magaro.
Vilevile Magaro amewataka wananchi wa mji huo wa Katoro kuendelea kupanda miti kila wanapofanya ujenzi katika makazi yao ili kuyatunza mazingira.
Kwa Upande wao Waheshimiwa Madiwani wa Kata za Katoro na Ludete ambao wameshiriki zoezi hilo wamempongeza Mkurugenzi Mtendaji pamoja na Watumishi wa Halmashauri ya Geita kwa namna ambavyo wameratibu zoezi la usafi katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Katoro.
" Nimpongeze Mhe Mkuu wa Wilaya kwa namna ambavyo ameelekeza usafi ufanyike katika mji wa katoro na Ofisi ya Mkurugenzi kwa hamasa kubwa iliyofanywa na wananchi kujitokeza kwa Wingi" Amesema Mhe Kigongo Benedicto Diwani wa Kata ya Katoro.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ludete Mhe Sebastian Benedicto amesema mji wa katoro ni mji unaokuwa kwa kasi na kuwataka wananchi kuwa Mabalozi wa Usafi kuanzia Majumbani hadi maeneo yao ya kazi.
Zoezi la kafanya Usafi wa Mazingira ni endelevu katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita na kila Jumamosi ya kila Mwisho wa mwezi wananchi hujitokeza kufanya usafi kwa pamoja katika mazingira yao katika kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuhakikisha mazingira yana kuwa safi na Salama.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa