Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mh. Stephen Wasira amewataka wananchi kudumisha amani pamoja na kutokujihusisha na vurugu haswa kipindi hichi ambacho nchi inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza na wakaazi wa Wilaya ya Geita kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Kakubilo mapema wiki hii katika sherehe za kuelekea Maadhimisho ya Miaka 48 ya CCM, Mh. Wasira amewataka wananchi kushikamana na kuelewa kuwa demokrasia sio fujo, bali kufanya siasa zenye mlengo wa kuleta maendeleo.
"Tunapaswa kuelewa kua maendeleo ni mchakato. Hivyo haiwezekani kufanya kila kitu kwa siku moja. Kama wananchi tunatakiwa kuelewa kuwa demokrasia sio fujo na hivyo tujitahidi kudumisha amani tuliyokuwa nayo." Amesema Mh. Wasira.
Aidha, Mh Wasira pia alipongeza juhudi za serikali chini ya Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuhakikisha zinaongeza shule za sekondari kwa watoto wakike kwenye kila mkoa, hivyo kuongeza nafasi kwa wasichana kujiendeleza kimasomo.
Kuhusiana na yaliyopitishwa kwenye Mkutano Mkuu uliofanyika hivi karibuni jijini Dodoma, Mh. Wasira alidokeza kuwa CCM imeridhia kufanya mabadiliko ya katiba ya Chama ambapo Mabalozi wa nyumba kumi, pamoja na kamati zao za wajumbe wataruhusiwa kupiga kura ili kuwachagua viongozi watakaokiwakilisha Chama kwenye Uchaguzi Mkuu.
Februari 5 mwaka huu ni kilele cha Maadhimisho ya miaka 48 ya Chama Cha mapinduzi (CCM), ambacho kiliasisiwa mwaka 1977, baada ya muungano wa vyama vya TANU kutoka Tanzania Bara na Afro-Shiraz Party (ASP) kutoka visiwani Zanzibar.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa