Agosti 20,
WARATIBU lishe nchini wamesisitizwa kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa akina mama wajawazito ili kuwasaidia kujifungua salama, pamoja na kupunguza madhara ambayo yanaweza kuwakumba watoto wachanga baada ya kuzaliwa.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyoendeshwa kwa siku mbili kwa Waratibu wa Lishe wa vituo vya kutolea huduma za afya, yakijumuisha vituo 13 vya Wilaya ya Geita vijijini, Afisa Lishe wa Mkoa, Bi Naomi Andrea Rumenyela amewataka wahudumu hao kuweka mkazo wa lishe bora kwa akina mama wajawazito pamoja na kuhakikisha wanatembelea vituo vya afya mara kwa mara pindi wanapojigundua kuwa ni wajawazito.
Aidha Bi Naomi pia amewataka wahudumu wa afya kuhakikisha wanajaza kwa usahihi taarifa za akina mama wajawazito, (Maoteo) kwenye vituo vyao ili dawa zinazotolewa kwa wajawazito ziweze kukidhi haja ya wajawazito ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya kina mama wanaopatwa na tatizo la ukosefu wa damu ya kutosha pindi wanapojifungua.
"Hakikisheni wakati wa kujaza taarifa za akina mama wajawazito, mnaweka taarifa sahihi kwenye mfumo ili Bohari ya Dawa ya Taifa (MSD) wanapotoa dawa, ziweze kuwafikia kama mlivyoagiza ili kupunguza tatizo la wajawazito wanaopoteza maisha kutokana na upungufu wa damu."Amesema Bi Naomi.
Afisa Lishe wa Mkoa, Bi Naomi Andrea Rumenyela akiwaelezea Waratibu Lishe kutoka Wilaya ya Geita kuhusiana na lishe bora kwa akina mama wajawazito ili kuepukana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kujifungua.
Pamoja na hayo, Bi Naomi pia amewataka waratibu hao wa lishe wahakikishe wanawahimiza akina mama waonyonyesha kuwapatia watoto wao maziwa ya mama, ambayo yana protini yakutosha, ikilinganishwa na maziwa mbadala ya ng’ombe.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Nasim Ginga amesema kuwa, wahudumu wa afya wanapaswa kuandika dawa zinazotumiwa na wajawazito, pamoja na kujaza kwa usahihi kitabu cha afya ya mtoto, kwa kuzingatia urefu, uzito na umri wa mtoto husika, ili taarifa zinazoletwa kutoka vituoni ziwe sahihi.
Vilevile Bi Nasim amewashauri Waratibu Lishe kuhusiana na kufanya tathmini ya kina ya hali ya lishe na ulaji wa mama wajawazito kabla, na baada ya kujifungua. "Ni muhimu kwa sisi kama wahudumu wa afya kupata taarifa za mlengwa kuhusu chakula anachotumia, mwenendo wa ulaji, na ni wakati gani hua anakula. Hii itasaidia kutokomeza changamoto ya utapiamlo miongoni mwa wajawazito, pamoja na watoto." Amesema Bi Nasim.
Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Nasim Ginga akitoa ufafanuzi kuhusu umuhimu wa Waratibu Lishe kuhakikisha wanajaza taarifa kwa usahihi za mama na mtoto wakiwa vituoni.
Kwa upande mwingine Mratibu wa Lishe kutoka kituo cha afya Nzera, Bwana Charles Kafulela amesema kuwa, kama wahudumu wa afya, wameweza kupata elimu ya kutosha kuhusu afya ya mama na mtoto ambayo itasaidia kukabiliana na changamoto za kiafya zinazoweza kujitokeza pindi mama akikosa lishe bora.
"Mafunzo yapo vizuri na tumeweza kupata vitu vingi ambayo tutavihitaji tukiwa kazini, pamoja na kujifunza vitu gani mama anapaswa kufanya ili kuwa na damu ya kutosha, pamoja na kuwa na afya bora yeye na mtoto ajaye."Amesema Bw Kafulela.
Baadhi ya Waratibu Lishe kutoka vituo vya afya tofauti Wilayani Geita waliojitokeza kwenye mafunzo yaliyolenga kuwapatia ujuzi zaidi kuhusiana na kutatua changamoto zinaweza kujitokeza kwa wazazi na watoto kutokana na lishe isiyo bora.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa