Wanafunzi waliomaliza mitihani ya kidato cha nne 2024 katika shule ya Sekondari Bugalama Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Novemba 26, 2024 wamejumuika pamoja na walimu na viongozi wa chama na serikali katika zoezi la upandaji wa miti na uchangiaji wa damu salama.
Awali akizungumza katika zoezi hilo Mkuu wa shule ya Sekondari Bugalama Mwl Gibson Petro Mkomi amesema shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 616 inazingatia misingi ya utoaji elimu bora, nidhamu kwa walimu na wanafunzi na utunzaji wa mazingira.
“Wanafunzi wetu waliomaliza kidato cha nne mwaka huu 2024 wameona watoe zawadi ya upandaji wa miti katika kutunza mazingira na kuchangia utoaji wa damu salama ili kusaidia jamii ambayo inapitia changamoto za upatikanaji wa damu.
Wanafunzi wakisikiliza elimu juu ya uchangiaji wa damu, kutoka kwa Afisa Mteknolojia maabara kitengo cha Damu salama Hospitali ya wilaya - Nzera
Aidha Mwalimu Mkomi amesema shule hiyo inazingatia utunzaji wa mazingira ikiwa ni sehemu ya kuunga juhudi za Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika upandaji wa miti ili kutunza mazingira .
“Tumeandaa miti 500 ambayo kati ya hiyo miti 100 ni miti ya matunda, 100 miti ya kivuli na miti 300 ya mbao ambayo imekuwa ikisaidia kutengeneza samani za shule pamoja na kuongeza pato la shule kipindi inapovunwa.” Ameongeza Mwl Mkomi.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bugalama, Mwl Gibson Mkomi akiongoza zoezi la upandaji miti katika shule ya Bugalama
Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalum Mhe Veronica Migelegele amewataka wanafunzi na walimu kuitunza miti waliyoipanda ili kuendelea kuunga juhudi za Mhe Rais za utunzaji wa Mazingira na kuwataka kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024”
“Tuyatunze mazingira na tushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili tupate viongozi bora kwa ajili ya kuongoza katika maeneo yetu na kuchochea maendeleo.” Amesema Mhe Migelegele
Diwani wa Viti Maalum Mhe Veronica Migelegele akizungumza mbele ya wananchi na wanafunzi waliojitokeza katika zoezi la upandaji wa miti na uchangiaji wa damu salama.
Wanafunzi hao wameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaboreshea mazingira mazuri ya kujifunzia ndio maana wameweza kurudi shuleni licha la kumaliza mitihani ili kuungana na wanafunzi wenzao wa vidato vya chini katika kupanda miti na kuchangia damu.”Tumepanda miti ili kuendelea kuboresha mazingira mazuri ya shule yetu pamoja na kuzuia mmomonyoko wa udongo ambao unaweza kuleta athari katika maeneo yetu. Amesema Dionizi Katisho mwanafunzi aliyehitimu kidato cha nne.
Pamoja na zoezi hilo wanafunzi hao, walimu pamoja na viongozi wa chama na serikali walioshiriki katika upandaji wa miti, wamechangia utoaji wa damu salama lililoratibiwa na watoa huduma kutoka Hospitali ya Wilaya iliyopo Nzera.
Zoezi la upandaji wa miti likiendelea katika shule ya sekondari Bugalama
Akizungumzia umuhimu wa kuchangia damu, Afisa Mteknolojia Maabara kitengo cha damu salama kutoka Hospitali ya Wilaya ya Geita-Nzera, Bi Petty Mzumbwe amesema upo umuhimu wa jamii kuchangia damu kwa kuwa hakuna kiwanda cha kuzalisha damu kuwasaidia wagonjwa wenye uhitaji katika maeneo mbalimbali nchini.
zoezi la uchangiaji wa Damu salama.
Shule ya Sekondari Bugalama ilianza mwaka 2009 na imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ambapo kwa mwaka 2023 iliweza kuwa ya kwanza na kuongoza kati ya shule 44 za Serikali kwa matokeo mazuri katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa