Wananchi wa kata ya Bugalama katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita wameishukuru Serikali kwa kuwajengea kwa kiwango cha changarawe, barabara ya Lwenge,Nyamikoma hadi Bugalama yenye urefu wa Kilomita 22.
Wakiongea katika ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Bw.Mathias Said na Mdo Paulo wameishukuru Serikali kwa barabara hiyo ambayo haikuwahi kujengwa tangu Uhuru huku wakieleza kuwa, kwa vile wengi wao ni wakulima itawasaidia sana kusafirisha mazao yao kuelekea Mjini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Bw.Barnabas Mapande amewataka wakala wa barabara Vijijini TARURA kuhakisha wanawafikia wananchi na kuwapatia elimu ya kuacha kufanya shughuli za kibinadamu umbali wa Mita 30 kutoka barabarani kama sheria inavyoelekeza ili kuepuka migogoro hapo Serikali itakapoamua kuzipanua barabara hizo.
Kauli hiyo imekuja kufuatia kuonekana kwa changamoto hiyo katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ambapo wananchi wameonekana kufanya shughuli za kilimo karibu na barabara ambapo hata wanachi wa Kata Bugalama wamesema kuwa wako tayari kupisha huku Bw.Said Mathias Mwenyekiti wa Ccm tawi la Bugalama akiomba kuwekwa alama zinazoonyesha mwisho wa hifadhi za barabara.
Akizungumzia Mradi huo Meneja wa TARURA Wilaya ya Geita Eng.Bahati Subeya amesema kuwa barabara hiyo iliyotengewa kiasi cha shilingi milioni 500 inatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu ambapo kukamilika kwake kutawasaidia wananchi wa kata ya Bugalama wasiwe wanazungukia Nzera ambako ni mbali zaidi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa