Wananchi mkoani Geita hasa makundi maalumu,wameshauriwa kuitikia chanjo ya Korona inayotolewa kwenye vituo vya Afya vilivyoainishwa, ili kupunguza hatari zaidi, kwa kuwa Serikali haitaki wananchi wake wadhurike.
Ushauri huo umetolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt.Jimmy Mtabwa, wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari ya hatua za kukabiliana na virusi vya Korona, na faida za chanjo ya ugonjwa huo.
Dkt.Mtabwa amesema kuwa Serikali imejiridhisha kuwa chanjo ya Johnson and Johnson inayotolewa hapa nchini ni salama kwa matumizi ndio maana inaruhusiwa kutumika, huku akisisitiza kuwa ni jukumu la Serikali yoyote kuwalinda watu wake, hivyo Serikali ya Tanzania haiwezi kutoa chanjo yenye madhara kwa wananchi.
Bw.Stephen Mhando Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa GGML akizungumza katika Mafunzo hayo.
Amesisitiza kuwa zipo tafiti za kisayansi zinazoonyesha kuwa,mtu aliyechanjwa hata ikitokea akapata maambukizi ya Korona,hawezi kuathirika kama ambavyo anaweza kuathirika mtu ambaye hajapata kabisa chanjo hiyo.
Aidha Dkt.Mtabwa akiwa kama Mwezeshaji katika mafunzo hayo kwa waandishi wa habari,ameendelea kutoa elimu ya njia sahihi za kujikinga na Korona,kwa kuwataka wananchi kufuata taratibu zinazoshauriwa na wataalamu wa Afya, ikiwemo kutokuvaa barakoa moja kwa zaidi ya masaa manne.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mh.Wilson Shimo akiwa katika picha ya Pamoja na Waandishi wa habari wa kituo cha Redio Rubondo fm 105.3 Kinachomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Mafunzo hayo ya Chanjo ya Korona kwa Waandishi wa Habari yamelenga kuongeza mwitikio wa chanjo kwa wananchi kupitia elimu watakayoipata katika vyombo hivyo, kwa kuwa ukimuelimisha mwandishi wa habari umeielimisha jamii.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa