Na: Hendrick Msangi
Wananchi wa kisiwa na kata ya Izumacheli Wilayani Geita, wamekumbwa na changamoto ya kushindwa kupeleka mazao ya samaki pamoja na biashara zingine kutokana na kivuko cha MV Tegemeo kuwa na safari moja hivyo kupelekea adha na shida ya usafiri katika maeneo yao.
Baadhi ya wananchi wa eneo hilo wameeleza kuwa, pamoja na uwepo wa kivuko hicho lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya usafiri kutokana na kwamba usafiri huo umekuwa ukisafirisha abiria mara moja kwa siku na kupelekea kusimama kwa baadhi ya shughuli.
Aidha, wananchi hao wameeleza kuwepo kwa changamoto ya mawasiliano hususani katika miundombinu ya usafiri na ucheleweshwaji, hivyo wanahitaji vivuko na usafiri wa njia ya maji ili kurahisisha shughuli mbalimbali na kufika katika maeneo mengine kwa wakati, Kutokana na jiografia ya eneo hilo pia wameomba kuwepo kwa vivuko vya kujitosheleza kutokana na mahitaji yao
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Mhe Fadhili Maganya amewataka watumishi na viongozi wilayani Geita kutoka kwenye ofisi zao na kwenda kuwasikiliza wananchi ili kutatua kero zao badala ya kusubiri viongozi wa kitaifa kufika.
Akizungumza katika Mkutano wa hadhara kufuatia ziara hiyo ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa,Diwani wa kata ya Izumacheli, Mhe Cosmas Fideli amekiri kuwepo kwa changamoto ya usafiri wa kivuko hicho, na kueleza kutokana na shida hiyo wananchi wanakosa huduma kwa wakati na kupelekea shughuli za uchumi kusimama kutokana na kushindwa kupeleka bidhaa sokoni kwa muda unaohitajika kutokana na kivuko hicho kufanya safari zake mara moja kwa siku. Pia ameongeza kuwa kuna baadhi ya vijiji havina kivuko na inawabidi kutumia mitumbwi midogo ambayo inahatarisha usalama wa wananchi.
Kufuatia kilio hicho Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita, Barnabas Mapande amemuomba Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Mhe Fadhili Maganya kuwasaidia kufikisha kilio hicho cha wananchi ili kiweze kutatuliwa kutokana na shida ya kivuko inayowakabili, na kuiomba TEMESA iweze kuwasaidia kutatua changamoto hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini Mhe Joseph Msukuma ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuletea fedha nyingi za miradi katika Wilaya ya Geita ikiwepo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami umbali wa kilometa 20 kutokea kutokea Kata ya Nkome hadi kijiji cha Sungusira kata ya Nzera.
Aidha, Mbunge wa jimbo la Geita Vijijini Mhe Joseph Msukuma ameahidi kulishughulika tatizo hilo, na kueleza kuwa Serikali imelipokea na inalifanyia kazi suala hilo, na kusema daraja la Busisi litakapokamilika vile vivuko vitapelekwa katika kisiwa hicho ili kukidhi mahitaji ya wananchi hao, na kuwahakikishia wananchi wa kisiwa hicho kuwepo kwa safari mbili hadi tatu kwa siku ili kutatua changamoto ya wananchi ya kukosekana kwa kivuko kwa wakati kwasababu kivuko kilichopo kinapita mara moja tu kwa siku.
Akiendelea na ziara hiyo Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wazazi Taifa aliitembelea kata ya Nkome ambayo wakazi wake wengi hujishughulisha na uvuvi ambapo alisikiliza kero za wananchi na kuwataka watumishi kuwatembelea wananchi ili kusikiliza kero zao ili kuepuka kusubiri viongozi wa kitaifa kufika katika maeneo ya wananchi kwani zipo kero ambazo zinaweza kumalizwa pasipo viongozi wa kitaifa kufika.
Wananchi wa Kata ya Nkome wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Mhe Fadhili Maganya ambapo walieleza kero zao na kupatiwa ufumbuzi
Pamoja na hayo aliigaza ofisi ya Mkuregenzi Mtendaji kufuatilia swala la ardhi kwa ajili ya upatikanaji wa eneo la kujenga mradi mkubwa wa soko la samaki pamoja na uwepo wa askari polisi wa kike katika kituo cha polisi kwenye kata ya Nkome.
Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilayani Geita na Watumishi wa Halmashauri wakiwa kwenye Mkutano wa Hadhara wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mhe Fadhili Maganya alipofanya ziara Wilayani Geita katika kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Wakati huo huo Mbunge wa jimbo la Geita Vijijini Mhe Joseph Msukuma aliishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipendelea Geita kwa kutoa fedha nyingi za miradi ukiwepo mradi wa kituo cha Afya Nkome ambao utakapokamilika wananchi wa kata hiyo watanufaika na huduma za afya ikiwa ni pamoja na urefu wa barabara kwa kiwango cha lami kilometa 20 kutokea Kata ya Nkome hadi kijiji cha Sungusira kata ya Nzera.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa