Timu ya Msaada wa Kisheria ijulikanayo kama Mama Samia Legal Aid Compaign (MSLAC ) imeendelea na Kampeni ya utoaji wa elimu ya msaada wa kisheria katika Kata ya Magenge Halmashauri ya Wilaya ya Geita Januari 29,2025.
Timu hiyo imetembelea Shule ya Sekondari Magenge yenye Jumla ya wanafunzi 450 wanaume wakiwa 264 na Wasichana 186 na shule ya Msingi Magenge yenye Jumla ya wanafunzi 904 Wavulana wakiwa 465 na Wasichana 439.
Wanafunzi hao wamepewa elimu juu ya Ukatili wa Kijinsia na Haki za Watoto na wametakiwa kutoa taarifa za unyanyasaji pale wanapo ona viashiria vya unyanyasaji.
"Kesi za Ukatili zimepewa kipaumbele na zinashughulikiwa zikiwepo kesi za ubakaji, hivyo mtoe taarifa mapema pindi mnapopitia hali yoyote ya ukatili katika maeneo yenu" Amesema Koplo Salome kutoka dawati la Jinsia Geita.
Aidha WP Salome amewaasa wanafunzi hao kuepukana na tabia za mahusiano ya kimapenzi wawapo shuleni kwani tabia hizo zinakatisha ndoto zao.
Akizungumza kuhusu haki za watoto Mhe Doreen ambaye ni Wakili kutoka Chama cha Mawakili Tanzania (TLS) amewakumbusha wanafunzi hao juu ya haki zao ikiwa ni pamoja na haki ya kulindwa.
" Serikali imewekeza miundombinu ya kuwalinda ili msiharibikiwe" Amesema Wakili Doreen.
Aidha wakili huyo amewataka watoto hao kuziishi ndoto zao na kuepuka watu ambao wanakatisha ndoto zao na kuwataka kujilinda kuanzia nyumbani.
"Anzeni kujisimamia kuanzia sasa ili mfikie malengo yenu kwa kuepuka kujihusisha na kazi ambazo zinahatarisha maisha yenu. Muwe na uhuru wa kutoa taarifa mapema ili kujisaidia" Ameongeza Wakili.
Kwa upande wao wanafunzi wa shule ya Sekondari Magenge wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutambua changamoto wanazopitia na kuwaletea huduma ya msaada wa kisheria.
Ngasani Forodhani na Edwin Evaristi ni wanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo, wameeleza ukatili uliopo majumbani unaotokea kati ya wazazi na kutaka kujua sehemu ya kupata msaada huku wakionyesha hali ya wasiwasi iwapo wazazi watapelekwa jela pindi wanapotoa taarifa za ukatili unaotokea majumbani.
" Mzazi ikitokea akifungwa itakuwa kama laana kwetu kwa kuwa tumetoa taarifa na jambo hili linatufanya kuwa na wasiwasi na kusababisha kuwa na uoga kutoa taarifa za ukatili." Amesema Ngasani
" Ninayo furaha kwa sababu Serikali inatukumbuka sisi wanafunzi ila wazazi wamekuwa sehemu ya kukwamisha ndoto zetu na tunakuwa na wasiwasi kutoa taarifa kwa walimu juu ya wazazi wanao tufanyia vitendo vya ukatili " Amezungumza kwa hisia Erick Evaristi mwanafunzi wa kidato cha nne.
Akiwatoa wasiwasi wanafunzi hao, WP Salome ametaka wanafunzi hao kutoa taarifa kwa watu wanao waamini huku akitoa wito kwa walimu kuwasaidia wanafunzi juu ya changamoto wanazopitia.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari Magenge Mwl.George Mgaya ameishukuru Timu hiyo kwa kutembelea shule ya Magenge kutoa elimu ya Ukatili wa Kijinsia na Haki za Watoto na kusema shule hiyo ni miongoni mwa shule sita zinazotekeleza mpango wa Elimu salama Mkoani Geita.
Zoezi la utoaji wa elimu juu ya msaada wa kisheria kwa wananchi linaendelea na jumla ya kata 10 zinatarajiwa kufikiwa na Timu hiyo ya Mama Samia Legal Aid Compaign (MSLAC )
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa