Wito umetolewa kujiunga na huduma ya M-Kilimo (mobile kilimo),jukwaa la mawasiliano linalowawezesha wakulima ,wafugaji,wavuvi,na wafanyabiashara mbalimbali kutangaza bidhaa,kutafuta masoko,na kupata ushauri mbalimbali kwa kutumia simu ya mkononi.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 17 na Afisa Kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Bw.Malick Lugemalila Athuman, ambapo amesema kuwa Teknolojia hii (mobile kilimo) imelenga kuwasaidia wakulima ,wafugaji,na wavuvi waweze kuyafikia masoko hasa hasa wanunuzi wa bidhaa na mazao ya kilimo pasipo kupitia adha ya kuyasafirisha mazao hayo kwenda sokoni.
Bw.Malick amesema kuwa jukwaa hili lina sehemu kuu mbili, ambayo ni huduma ya masoko, sehemu ambayo inawaunganisha wauzaji na wanunuzi kuuza na kununua mazao,na sehemu ya pili ni huduma ya ushauri, ambayo ni sehemu ya kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa maafisa ugani.
Amesema kuwa takwimu zinaonesha watu karibu milioni arobaini na tatu wanamiliki simu za mkononi ,hivyo ni fursa nzuri kwa taasisi za serikali na wadau kuitumia, katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii, ikiwemo kuyafikia masoko ya mazao ya kilimo,mifugo na uvuvi.
Akielekeza namna ya kujiunga na huduma hii amesema kuwa, hatua ya kwanza katika simu ya mkononi Unaenda uwanja wa kuandika namba ya simu unabonyeza, *152*00# kisha unabonyeza namba 7 ambayo ni kilimo,ufugaji kisha unabonyeza namba 2 ambayo ni M-Kilimo.
Aidha baada ya hapo unaenda kwenye Menyu ya kujisajili, ambapo mtumiaji ataandika Jina lake kamili, kijiji,kata,wilaya na mkoa anapopatikana,ambapo baada ya hapo mtumiaji atakuwa amejisajili na atapata menyu ya kuuza mazao na kununua, bei za mazao na ushauri wa kitaalamu wa kilimo,mifugo na uvuvi kutoka kwa Afisa ugani wa eneo lake, kwa kutumia menyu ya kuomba ushauri.
Aidha amewakumbusha pia wakulima kuwa karibu na wataalamu wa kilimo, ili waweze kupata ushauri wa mbegu bora na pembejeo mbalimbali za kilimo hasa katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya wa kilimo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa